Home Habari za michezo KIBADENI: TATIZO SIMBA SIO KOCHA …NI WACHEZAJI….,WANASAJILI KWA KUANGALIA MAJINA…BOCCO NA KAGERE...

KIBADENI: TATIZO SIMBA SIO KOCHA …NI WACHEZAJI….,WANASAJILI KWA KUANGALIA MAJINA…BOCCO NA KAGERE WAENDE…


Nyota wa Simba, Pascal Wawa, Chris Mugalu, John Bocco na Meddie Kagere wamependekezwa wapewe mkono wa kwaheri msimu huu, huku timu hiyo imeshauriwa kutosajili kwa majina kwenye usajili wa msimu huu wa dirisha kubwa.

Nyota wa zamani wa timu hiyo wameeleza mtazamo wao kwenye usajili wa klabu hiyo, ambayo msimu huu imeshindwa kutetea ubingwa wa FA na ina nafasi kubwa ya kukosa Ligi Kuu, taji walilolitwaa kwa misimu minne mfululizo.

Matokeo ya Simba ambayo ipo kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya vinara, Yanga, yamewaibua nyota wake wa zamani ambao walisema jambo pekee litakalowabeba msimu ujao ni usajili makini.

“Wasiangalie majina, wasajili timu kulingana na mahitaji,” alisema nyota na kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah ‘King’ Kibaden, ambaye alisisitiza kilichoikwamisha Simba kutetea mataji yake msimu huu si kocha, bali ni aina ya wachezaji ilionao.

Kauli sawa na iliyotolewa na kipa wa zamani wa timu hiyo, Mosses Mkandawile, ambaye alisema kuna baadhi ya wachezaji Simba inapaswa kuwapa mkono wa kwaheri akiwamo Wawa, Mugalu, Bocco na Kagere.

“Bocco na Kagere ni kwa sababu ya umri, Wawa pia umri umesogea hivyo akikutana na mshambuliaji anayekimbia lazima ataachwa na Mugalu msimu huu hajaisaidia timu,” aisema Mkandawile.

Alisema mahitaji makubwa ya Simba kwenye usajili ujao ni kwenye eneo la ushambuliaji, ambako wanahitaji kupata mchezaji ambaye atawapa uhakika wa mabao bila presha.

“Tunao Kagere, Mugalu na Bocco ambao msimu huu wote uwezo wao haukuwa mzuri, vilevile Kapombe (Shomari) anapaswa apate mtu wa kumsaidia, tusajili beki wa kulia mwenye kiwango cha kuitumikia Simba,” alisema Mkandawile.

Alisema timu hiyo inapaswa kusajili beki wa kati mzuri, ambaye ukiachana na Onyango na Inonga, atakuwa na mchango mkubwa kwenye timu.

“Kama nilivyosema Wawa umri wa mpira umesogea kidogo, hivyo anapokutana na mikiki ni ngumu au akikutana na mtu mwenye spidi kufukuzana naye si rahisi,” alisema.

Aliongeza kuwa Simba haina shida kwenye eneo la kiungo, kuanzia katika ukabaji na hata kushambulia, shida ipo kwa mabeki na washambuliaji.

SOMA NA HII  MAOKOTO TIME NA HOT KENO YA MERIDIAN BET

Malota Soma, nyota mwingine wa zamani wa mabingwa hao mara 22 wa Ligi Kuu, alisema kwenye usajili wa msimu huu klabu isiangalie majina, bali uwezo wa mchezaji.

“Mchezaji anaweza kuwa mfungaji mzuri, lakini je anacheza na nani ambaye anamchezesha na kumpa pasi za kufunga, kama hakuna muunganiko mzuri pia ni shida, hivyo klabu wakati inasajili, ingezingatia hilo pia,” alisema.

Akitolea mfano yeye kusajiliwa Simba ni baada ya Zamoyoni Mogella, aliyekuwa mshambuliaji mahiri wa wakati huo kusajiliwa na klabu hiyo, akisema mtu anayesababisha afunge kwa kumchezesha ni Malota, hivyo klabu ikawasajili wote na matunda yalionekana.