Home Habari za michezo KUELEKEA MSIMU UJAO….NABI AOMBA SIKU 30 TU ZA KUFANYA KAZI YA KUITIKISA...

KUELEKEA MSIMU UJAO….NABI AOMBA SIKU 30 TU ZA KUFANYA KAZI YA KUITIKISA AFRIKA….ALIA NA MUDA…


Yanga tayari ina uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao na kocha Nasreddine Nabi amesema anahitaji kambi ya siku 30 tu.

Kutokana na kutotaka kupata aibu kama ya msimu uliopita kimataifa, kocha Nabi alisema kuwa, kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa kimataifa kama atapata siku 30 zitatosha kwake kuiandaa timu, lakini anapanga kufanya kikao kizito na wachezaji ambao atabaki nao.

Kalenda ya CAF inaonyesha msimu mpya wa michuano hiyo huenda ukaanza wiki kadhaa kabla au baada ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara kwa 2022-2023 na Nabi amepanga kuwajaza upepo wachezaji wake akitaka kila mmoja kuondoa hesabu za kupata mapumziko ya muda mrefu.

“Viongozi wangu hawapumziki, japo wamefanya kazi kubwa shida yangu ni wachezaji wangu, msimu huu wamefanya kazi kubwa sana iliyoshangaza hasa wakati huu ambao tunakaribia kuwa na mafanikio makubwa ya msimu kwa mashindano ya ndani,” alisema Nabi.

“Ukiangalia kalenda ya CAF utaona muda wa kuanza msimu mpya ujao hauko mbali kutoka pale ligi na mashindano ya ndani yatakapomalizika, angalia tutacheza fainali Julai 2 ina maana kuanzia Julai 4 vijana wanatakiwa kuruhusiwa kupumzika ila muda huo hautatosha sana.

“Msimu uliopita hatukufanya vizuri kwa kuwa tulipata muda mfupi na changamoto nyingi katika maandalizi ya msimu mpya haikuwa kitu kizuri kwa wachezaji wenye malengo ya kwenda mbele, nitawaambia ni bora tuumie sasa ili tuwe na kitu kizuri baadaye kisha tutapumzika. Nafikiria kama watakubaliana nami nitawapa mapumziko Novemba au Desemba pale ili waweze kupumzisha akili kidogo.”

Nabi alisema ameamua kutumia siku 30 badala ya zile 44 ambazo zilitakiwa kiutaratibu.

“Kikawaida tulitakiwa kuwa na wiki sita lakini kama unavyoona ligi za ndani zimechelewa sana kumalizika hapa hakuna muda wa kuanza kulalamika ni lazima tubadili yale tuliyoyanga, nafikiria kuhitaji muda wa wiki nne tu ili tuweze kujiandaa vyema.

“Nafurahia uongozi ulianza kuliona hili na kuna mambo ya kuanza kutafuta wachezaji wapya, walishaanza mapema hii itatusaidia sana tuweze kujikusanya kwa wakati ili tuanze maandalizi kwa pamoja kwa msimu mpya na kuendelea kuwapa raha mashabiki wetu,” alisema kocha huyo.

SOMA NA HII  KOCHA WA TIMU YA TAIFA YA MOROCCO AMPIGA KIKUMBO BENCHIKHA CAF