CEDRIC Kaze, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa jambo litakalomuongezea kasi mshambuliaji wake Michael Sarpong pamoja na Yacouba Songne kutupia mabao mengi ni kupokea mipira kutoka pembeni na kati kutoka kwa viungo wake.
Sarpong na Yacouba ambao ni washambuliaji kwa pamoja wamehusika kwenye jumla ya mabao 12 kati ya 29 yaliyofungwa na timu hiyo inayoongoza ligi ikiwa na pointi 44 baada ya kucheza mechi 18.
Sarpong ametupia mabao manne sawa na Yacouba ambaye ana pasi nne za mabao wote ikiwa ni msimu wao wa kwanza kuwa ndani ya kikosi cha Yanga.
Kaze amesema kuwa kazi ambayo amewapa viungo wake wa pembeni ambao ni Farid Mussa na Carlos Carlinhos ni kutoa mipira kwa kuugawa uwanja.
“Sasa nimegundua tatizo ni kwamba washambuliaji wanakosa mipira ya kuijaza nyavuni kwa kuwa inatoka upande mmoja, nimewaambia viungo wangu kuwa waugawe uwanja kwa kutoka pembeni na kati pia.
“Ikiwa watatoa pasi kutoka pembeni na wengine watatoa pasi kutoka katikati itaongeza hali ya washambuliaji kuwa kwenye nafasi nyingi uwanjani na kufunga namna ambavyo wanataka na inawezekana,” amesema.
Kesho, Februari 13, Yanga itamenyana na Mbeya City, Uwanja wa Sokoine ikiwa na kumbukumbu ya kushinda kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa.