Home Azam FC LWANDAMINA: MAJERUHI HAYATUTISHI

LWANDAMINA: MAJERUHI HAYATUTISHI


LICHA ya nyota wa kikosi chake kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara kocha mkuu wa klabu ya Azam, George Lwandamina amesema kwamba hali hiyo haiwezi kuwa kikwazo kwao katika kuhakikisha wanafanikisha malengo yao msimu huu.

Tangu kuanza kwa msimu huu, Azam imekuwa ni miongoni mwa timu ambazo zimeripoti kesi nyingi za wachezaji wao kupata majeraha.

Azam kwenye mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union ilishuka uwanjani katika dimba la Mkwakwani jijini Tanga huku ikikosa huduma ya nyota wake wanne ambao ni; Obrey Chirwa, Emmanuel Charles, Frank Domayo na Abdul Omary.

Akizungumzia hali ya majeraha ndani ya kikosi chake, Lwandamina alisema: “Mpira ni mchezo unaotumia mwili, hivyo huwezi kupinga uwepo wa wachezaji wenye majeraha kwenye kikosi chako.

“Kuna wakati baadhi ya wachezaji muhimu watapata majeraha na kushindwa kucheza, wengine itawalazimu kucheza wakiwa na majeraha.

“Hivyo hilo ni suala la kawaida kwenye soka na haliwezi kuwa sababu ya kutuharibia mipango yetu kama timu, bali tutaendelea kupambana kuhakikisha tunafanya vizuri ili kufikia malengo tuliyojiwekea,”

Kipigo dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliopita kimewafanya Azam kusalia katika nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi zao 33, walizokusanya katika michezo 19 waliyocheza mpaka sasa.

SOMA NA HII  AzAM FC YAPATA PIGO KUBWA...MCHEZAJI HUYU KUONDOKA...KUSAJILI MASHINE HII MPYA