OFISA Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa kikosi cha Simba kinatarajia kuwasili leo kwenye ardhi ya Tanzania huku akiwaomba mashabiki waendelee na shughuli zao wasijitokeze Uwanja wa ndege kuwapokea kwa kuwa jambo lao halijatimia.
Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi dhidi ya AS Vita ya Congo inayonolewa na Florent Ibenge.
Bao la ushindi kwa Simba inayonolewa na Didier Gomes lilifungwa dakika ya 60 na Chris Mugalu kwa penalti na kuwafanya wawakilishi hao kuanza kuongoza kundi A kwa kukusanya pointi tatu.
Jana,Februari 13 kikosi kilisepa Congo na kuibukia Addis Ababa ambapo leo kinatarajiwa kuunganisha safari na kuibuka Bongo majira ya saa 6 mchana.
Manara amesema kuwa wanatambua umuhimu na dua za mashabiki ila kwa sasa wawaache wachezaji wapumzike kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United pamoja na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ambao wapo nao kundi moja.
“Tumepokea salamu nyingi za ushindi ila mashabiki kwa sasa tunawashukuru sana kwa sapoti yao, kuhusu kutupokea kwa furaha bado, watuache kidogo bado kazi ni ndefu.
“Hatujafikia malengo yetu, ikifika wakati tunarudi na ubingwa, mataji pale na mambo mengine itakuwa rasmi kwa mashabiki kuja ila kwa sasa tunawaomba mashabiki muendelee na shughuli zenu, tunajua mnafurahi kuona tumeshinda nasi tunafuraha ila malengo yetu bado na safari bado ni ndefu,” .