Na Saleh Ally
WAKATI mechi kati ya Simba na AS Vita nilitaka kuwe na utulivu sana ili niweze kuangalia mambo kadhaa ya msingi na kubwa kwangu lilikuwa ni je, Simba walijifunza jambo kutokana na kile kipigo cha mabao 5-0 jijini Kinshasa miaka mitatu tu iliyopita.
Hofu kubwa kwangu, kwamba hata kama Simba walijifunza, nakumbuka walikuwa chini ya kocha Mfaransa, Patrick Aussems, baada ya hapo wakawa na Mbelgiji, Sven Vandenbroeck na mwisho wamerejea Kinshasa wakiwa na kocha mwingine Mfaransa, Didier Gomes, huyu ni mpya.
Kwamba wataweza, ingawa ni kwamba wachezaji wengi walikuwa ni hawahawa na hata kipa Aishi Manula ni yuleyule. AS Vita, tayari nilikuwa na taarifa haijapoteza mchezo takriban mwaka mzima. Kwangu soka ni burudani na kazi, nikasema nitajifunza huku nikiburudika kama ilivyo ada.
Ukaguzi wangu wa kwanza, ulianzia katika kikosi. Nikaona ni wachezaji wanne tu waliokuwa wamepata nafasi ya kuanza, kipa, mabeki wawili wa pembeni pamoja na kiungo mkabaji mmoja, si haba.
Baada ya mechi kuanza, nikaanza kuangalia namna ambavyo Simba walijipanga na kufanya mambo yaende. Nakumbuka katika mabao matano waliyofungwa, nakumbuka mipira mitatu ya adhabu na kona ndiyo iliwamaliza na wachezaji wa Simba hawakuwa wakiruka juu, wakafungwa mabao mepesi sana.
Katika mechi hiyo ya juzi, mambo yakawa tofauti na hakukuwa na nafasi ya mchezaji hata mmoja wa AS Vita kuruka peke yake. Kila adhabu na kona iliyoelekezwa kwa Simba, pale langoni ilikuwa hakuna kulala. Wazi nikajua Simba hili walilifanyia kazi na Gomes alishajua njia sahihi ya kupambana nalo.
Aina ya kupanga mashambulizi, Simba inajulikana. Aina ya ukabaki wa nguvu na utibuzi wa mashambulizi ikaonekana Simba kweli wamejipanga na binafsi nikasema kwa mwendo huu wanaweza wakaondoka hata na pointi moja badala ya kuamini wangefungwa mabao machache angalau mawili. Lakini mwisho, Simba wakaonyesha kweli walijifunza na sasa wamejipanga kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kwa namna Simba walivyocheza, hakuna ubishi tena ni timu kubwa Afrika. Hawakuwa wakiweweseka wala hofu ya kufungwa na badala yake walipambana kuzuia kuruhusu bao lakini wakatengeneza nafasi.
Hawakuonekana kama wako ugenini licha ya nidhamu kubwa waliyokuwa nayo kiulinzi na kimashambulizi. Walionyesha ni timu ya kiwango cha Afrika. Jambo ambalo ni gumu kuonekana kwa kuwa Watanzania tunapenda kujidharau.
Inawezekana kabisa kwa aina ya uchezaji wa Simba katika mechi hiyo na kama itaendelea hivyo katika mechi zijazo, basi wanakwenda kuwa gumzo barani Afrika. Kikubwa ni lazima waendeleze walichokianzisha.
Simba ni kubwa si kwa maneno tena na hasa unapozungumzia michuano hii mikubwa ya Afrika kwa ngazi ya klabu. Bila shaka hata Al Ahly sasa watakuja Dar es Salaam kwa tahadhari kubwa sana wakijua Simba si timu ya utaniutani tena.
Haina maana Simba haitakosea, au haitafungwa maana vigogo kama kina Ahly pia hufungwa na timu mbalimbali za Afrika. Simba walipofikia, Watanzania wanapaswa kujivunia na hakuna ubishi anayetaka kukua au kubadilika, Simba wanaweza kuwa mfano mzuri. Hapa ondoa mambo ya ushabiki, badala yake angalia au ujali mpira.
Jambo la kwanza, kwa misimu minne sasa, wameendelea kubaki na wachezaji walewale kwa asilimia 70. Wamekuwa makini katika uongezaji wa wachezaji wapya na sasa wanakwenda katika ile ndoto yao ya kuwa kigogo wa Afrika.
Tukubali, Simba wamepita hatua. Kama uko Tanzania na ukataka kuwabeza ni kujipiga vita mwenyewe. Utakuwa hautumii haki yako ya kujifunza kupitia chako au cha nyumbani kwenu, hapa nazungumzia kwa Watanzania. Hivyo, angalia hatua wanazopiga na unaweza kujifunza jambo likawa msaada katika kikosi chako.
Walichokifanya Simba kuifunga AS Vita pale Kinshasa, wametengeneza rekodi nyingine ambayo itadumu kwa muda mwingi, huenda wengine itakuwa vigumu kuwaelewa na hasa mwanzoni.
Lazima Simba wamejifunza kupitia misukosuko ya kufungwa tano mara mbili yaani Kinshasa na Ahly lakini leo, wameonyesha kuna mabadiliko yenye mafanikio, usikae nao mbali ili unyakue mambo.