Home Yanga SC DK MSOLLA ANAKUMBUSHWA MAKOSA WAKATI AKIWA PEMBENI YA USUKANI….

DK MSOLLA ANAKUMBUSHWA MAKOSA WAKATI AKIWA PEMBENI YA USUKANI….

 

Na Saleh Ally

MOJA ya sifa kubwa za wapenda mpira ni kutokuwa wakweli, kutopenda kuelezana ukweli na kupendelea kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa!

Bahati mbaya zaidi wale ambao hupenda kuwa wazi au kusema ukweli, ndio huonekana wabaya kwa kuwa soka ni mchezo uliozungukwa na watu wengi wanafiki ambao kazi yao ni kusema maneno ya uongo ili waishi.

Haiwezekani kukawa na mabadiliko kwenda katika mafanikio kama watu wataona kusema uongo au unafiki kuwapamba watu na kadhalika ndio maneno sahihi yanayoweza kuleta mabadiliko au mafanikio.

 Nimeona juzi, Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla akitolewa Uwanja wa Mkapa huku baadhi ya mashabiki wakisema maneno makali dhidi ya uongozi wa Yanga.

Mashabiki hao wameonyesha kukerwa na kikosi cha Yanga kupata sare ya nne mfululizo katika mechi yao dhidi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar.

Walipata sare dhidi ya Gwambina na Tanzania Prisons katika mzunguko wa kwanza, kisha kwenye mzunguko wa pili wakapata sare ya kwanza ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City wakiwa ugenini jijini Mbeya na hii ya juzi ya mabao 3-3 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, maana yake ndani ya mechi mbili, Yanga wamendondosha pointi nne.

Wako kileleni lakini wanajua kiasi gani wanahatarisha uongozi wao dhidi ya mabingwa watetezi, watani wao Simba ambao kama watashinda mechi tatu zilizobaki za viporo, wataizidi Yanga kwa pointi mbili na mabao ya kufunga pia.

Wakati mashabiki wakionekana kuudhiwa na hilo, hasira zao zinakwenda moja kwa moja kwa Dk Msolla kwa kuwa wanajua ndiye walimpa dhamana ya kuiendesha klabu yao, wana haki.

Hasira za kwamba kuna jambo haliendi vizuri na mhusika mkuu ni Dk Msolla. Kwangu taratibu naanza kujiuliza, kweli Dk Msolla anasajili? Tumewahi kuona akileta wachezaji na kuwasainisha? Jibu litakuwa hapana na ukweli hiki ni kitu Yanga wanakikosea na huenda watakasirishwa na kuambiwa lakini utafikia wakati watajifunza kupitia ninachoandika.

SOMA NA HII  KUHUSU MO DEWJI KUSHUKURIWA KWA YANGA KUTINGA ROBO CAF...HIVI NDIVYO KAMWE ALIVYOIJIBU HOJA HII..

Ukiangalia kwa undani unaona kwa kiasi kikubwa Dk Msolla pamoja na uongozi wake wanakosea, kiasi kwangu naweza kuhoji kwamba leo tunaweza tukawauliza usajili wao? Maana usajili wa Yanga unafanywa na wadhamini na si klabuni.

Usajili wa Yanga, unafanywa na nani? Sote tunajua na unaona viongozi hawashiriki na kama wanashiriki, wapi? Maana hata wakati wachezaji wakisajiliwa, wamekuwa hawaonekani na mara nyingi usajili haufanyiki katika klabu hiyo. Mara nyingi tunawaona wakiwa na wadhamini na si viongozi wanaohusika.

Lazima Wanayanga wawalalamikie viongozi au kuwalaumu kwa kuwa ndio waliowapa dhamana, sahihi. Lakini tujiulize, viongozi wanashiriki katika kilicho sahihi kwa maana ya klabu kwamba wanajua au kufanya kila kinachotakiwa?

Binafsi naona wadhamini wao wana nia nzuri lakini ukweli lazima viongozi wa klabu wawe na nguvu sahihi ya ushiriki wa mambo.

Unaona leo mashabiki wanalia na wao kwa kuwa wanajua ndio wanaofanya kila kitu. Ndani ya klabu wanashiriki yote, wao ndio wanaamua yote au hawana nguvu tena na uamuzi unafanywa na wengine.

Nimekuwa nikiiona shida Yanga hapo baadaye, ninaona watu wakitupiana lawama na ikiwezekana wadhamini kukwazwa jambo ambalo kama utaratibu mzuri utafanyika mapema unaweza kuokoa mengine yasiyo sahihi kutokea mbele.

Msiwaache Dk Msolla na Frederick Mwakalebela wawe watu wa kulaumiwa tu mwishoni lakini wakati wa utendaji wakawa wanafanya watu wengine wa kamati au wadhamini.

Dk Msolla na Mwakalebela, wote ni wazoefu katika mpira na ndio wana dhamana ya wanachama na mashabiki, basi wasimamie kile ambacho wamekabidhiwa kwa ubora ulio sahihi badala ya kufanya mambo ili mradi tu.

Nimesema mwanzo, hatuambiani ukweli na wengine wanahofia kusema watawaudhi watu fulani lakini ukweli ni hivi, Yanga ni timu ya Watanzania na tunapaswa kuambiana ukweli mambo yaende sawa kwa kuwa maendeleo ya klabu hiyo kongwe ni maendeleo ya mpira wa Tanzania.