IPO waza kwamba kwa msimu huu ni timu nne zitashuka kutoka Ligi Kuu Bara na zitashiriki Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu wa 2021/22.
Timu mbili zitacheza playoff ili kumsaka mshindi ambaye atabaki ndani ya ligi ama kushiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Kwa maana hiyo ni kwamba kwa msimu wa 2021/22 ni timu 16 zitashiriki ligi. Kwa kujua hilo ni muhimu kila timu ikapambana kusaka ushindi ndani ya uwanja.
Mzunguko wa pili ni muda wa hesabu na kukamilisha mipango iliyopangwa.Kazi ni moja kwa timu kusaka pointi tatu uwanjani.
Kikubwa kwa timu ambazo bado zipo nafasi ya chini kwa sasa ni lazima benchi la ufundi kutafuta mbinu mpya itakayowapa matokeo mazuri kwa mechi zao ndani ya ligi.
Msimu huu sio wa kitoto kwani kila timu inayoingia uwanjani inatambua nini inahitaji na inafanya vizuri kupata matokeo chanya.
Zipo pia ambazo zinapata matokeo kwa kusuasua jambo ambalo linanipa wasiwasi kwamba ikiwa hazitashtuka kwa wakati huu kazi itakuwa ngumu hapo baadaye itakapokuja kushtuka na kuanza kusaka ushindi.
Hakuna cha kupoteza kwa sasa kwa kuwa kila timu inaamini ipo ndani ya ligi na inaishi kwenye malengo yake. Kwa kulijua hilo ni muhimu kila mmoja akapambana kufikia malengo yake.
Kwa timu ambazo zinashiriki Ligi Daraja la Kwanza pia ni wakati wao kujipanga upya kuendeleza gurudumu la kusaka ushindi ili waweze kupanda mpaka kushiriki Ligi Kuu Bara.
Tukumbuke kwamba kupanda kwenye ligi ni ndoto za timu nyingi shiriki kwenye Ligi Daraja la Kwanza, mbinu pekee itakayoweza kufanikisha hilo ni juhudi isiyokuwa ya kawaida kwenye kusaka ushindi.
Ipo wazi kwamba kwenye suala la uchumi mambo bado sio mazuri kwa timu nyingi ila hapohapo ni pakuanzia kwa kuwa ili mdhamini apatikane lazima timu iwe inapata matokeo chanya.
Kwenye Ligi Kuu Bara kuna ushindani wa kupata ushindi na kinachopiganiwa huku ni kombe na kwa timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza zinahitaji kupanda mpaka kushiriki ligi.
Kitu kizuri ambacho kinahitajika ni kuona kwamba kila timu inapata matokeo ambayo yanastahili bila kuwa na mpango wowote wa kuyapanga na hasa wakati zinapokuwa nyumbani kucheza.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mbali na kuitazama Ligi Kuu Bara kwa ukaribu kuna umuhimu wa kutazama na mwenendo mzima wa Ligi Daraja la Kwanza.
Endapo jicho kubwa litakuwa ndani ya ligi pekee na kuacha huku kwenye kiwanda cha kutengeneza timu shiriki bila kujali maisha yao itakuwa ni hatari kwa afya ya soka letu.
Ili soka liendelee ni lazima kuwe na misingi makini ambayo inaanzia huku chini na haijengwi kwa kubahatisha bali mipango makini na hesabu zenye uhakika.
Timu shiriki ndani ya Ligi Daraja la Kwanza ni lazima zitambue namna gani zinaweza kufikia malengo yao. Mikakati makini itazipa matokeo mazuri na mwisho wa siku timu zitatimiza malengo yao.
Njia ya kupata ushindi ni moja tu kupambana na kufanyia kazi makosa yao ambayo yalipita kwenye mechi za nyuma ambazo matokeo yaliyopatikana hayakuwa rafiki kwa benchi la ufundi pamoja na wachezaji.
Ni safari ndefu ya kuvuka mlima wa Ligi Daraja la Kwanza na kuibukia ndani ya Ligi Kuu Bara ambayo nayo ushindani wake ni mkubwa.
Jambo la kuzingatia ni pamoja na nidhamu kwa wachezaji kwenye mechi zote bila kujali wanacheza na nani ni mbinu za kuwafanya wawe makini na bora kwenye matokeo ambayo wanayapata kwenye ligi.
Endapo hakutakuwa na nidhamu kwa wachezaji itasababisha wengi washindwe kufikia malengo kwani mchezo wa mpira ni kitu ambacho kinawategemea wachezaji na mashabiki nao wana mchango wao pia.
Kwa kuanza na kuwaheshimu wapinzani kutatoa picha mpya kwamba timu mnayokutana ni ngumu hivyo mtaingia kwa tahadhari na mwisho wa siku kile mnachokihitaji mtakipata.
Ikitokea mmoja kati yenu akaleta jeuri na kumdharau mpinzani wake adhabu yake ataipata ndani ya uwanja. Mpira sio kitu cha kuficha kila jambo linaonekana hadharani hivyo ikiwa utamdharau mpinzani wako matokeo yatakuhukumu.
Jambo la msingi kwenye mechi zijazo ni kufanyia kazi makosa yaliyopita na kuanza upya kwani kupoteza mchezo, kushinda na kupata sare haya ni matokeo ya kila timu shiriki ndani ya ligi zote.
Zile kelele ambazo zimekuwa zikiimbwa kwa wakati uliopita kwa sasa nazo zinapaswa zifanyiwe kazi kwa umakini na utulivu ili kuzipoteza kabisa.
Waamuzi ambao wanasimamia sheria 17 ni muhimu kutazama namna bora ya kuzidi kuwa bora na kuepuka lawama ambazo wamekuwa wakiachiwa.
Muda sahihi wa kutazama maamuzi ni kujifunza kupitia makosa na kukubali kuyaacha hasa pale ambapo inapotokea kwa bahati mbaya.
Makosa yapo kwa kuwa binadamu anafanya makosa ila inapotokea kila mara hili linakuwa sio kosa tena bali ni janga kwa kuwa hakuna ambaye anakuwa anajali.
Njia pekee ya timu kupata ushindi ndani ya dakika tisini ni kupambana ndani ya uwanja ili kupata ushindi kwa uhalali bila kujali aina ya timu ambayo unakutana nayo uwanjani.
Nafasi bado ipo kwa kila timu kusaka ushindi ndani ya uwanja na mashabiki pia ni muhimu kuendelea kutoa sapoti kwa timu zao pendwa.