Home Yanga SC KAZE AFUNGUKIA SABABU YA SARE MFULULIZO

KAZE AFUNGUKIA SABABU YA SARE MFULULIZO


KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, Cedric Kaze amefunguka kuwa, kukosa umakini kwa washambuliaji wake katikati kutumia nafasi wanazotengeza uwanjani, ndiyo sababu kubwa ya kupata matokeo ya sare mfululizo katika michezo yao miwili iliyopita.

Yanga Jumamosi ilitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City, sare hiyo ni ya pili mfululizo kwa Yanga kwenye Ligi Kuu Bara, ambapo waliingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons.

Licha ya sare hiyo dhidi ya Mbeya City, Yanga imeendelea kusalia kileleni mwa msimamo baada ya kujikusanyia pointi 45 katika michezo yao 19 waliyocheza mpaka sasa wakishinda mechi 13 na kutoa sare michezo sita.

Akizungumzia matokeo hayo Kaze amesema: “Imekuwa bahati mbaya sana kwetu kupoteza pointi nne katika michezo yetu miwili mfululizo iliyopita, hayakuwa malengo yetu na kwa maoni yangu nadhani tulipaswa kupata pointi sita katika michezo hiyo.

“Kwenye michezo yote miwili tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini tukashindwa kuzitumia, nadhani tunapaswa kurekebisha hilo katika michezo yetu ijayo.

“Bado tuna malengo ya kupambania ubingwa, na tutafanya kila jitihada kuhakikisha lengo hilo linatimia licha ya ushindani mkubwa uliopo,”

SOMA NA HII  MANARA AWATOLEA UVIVU TFF KISA CHAMA, AZIZ KI.... ISHU IKO HIVI