Home Ligi Kuu KUWENI MAKINI, SPORTPESA NA WENZAO WASIWAKIMBIE…

KUWENI MAKINI, SPORTPESA NA WENZAO WASIWAKIMBIE…

 Na Saleh Ally

KUENDESHA timu ya mpira na ikawa makini si jambo dogo hata kidogo na kiwango kikubwa cha fedha kinatakiwa.

Kiwango cha fedha pamoja na mipango madhubuti ndio kinachotoa dira ya timu inakwenda wapi.

Unaona Simba ilianza na bajeti ya Sh milioni 900 kwa mwaka, sasa wako zaidi ya Sh bilioni 4. Zaidi ya mara nne na hii ni ndani ya miaka mitano tu, ndio maana unaiona Simba tofauti na ile ya miaka hiyo iliyopita.

Utofauti wake unatokana na mwendo wa timu na fedha inatumika hasa. Hapa ndipo kunatakiwa kuwa na vyanzo sahihi vya uingizaji fedha ili kuifanya timu iweze kwenda na mambo yake kwa uhakika.

Katika soka, mambo hayawezi kuwa ya siri tena badala yake inajulikana wazi ili timu au klabu iingize fedha za kujiendesha inatakiwa ifanye nini.

Kwanza viingilio vya mlangoni ambavyo vitatokana na timu hiyo kuwa na mashabiki wengi ambao wataifanya iingize fedha nyingi. Baada ya hapo, ni fedha za wadhamini ambao wakiingiza fedha zao nao watapata nafasi ya kujitangaza kupitia kikosi cha timu husika chini ya klabu husika.

Mapato ambayo yatatokana na mauzo ya vifaa vya klabu hiyo kama jezi, bukta, fulana, vishika ufunguo na kadhalika na baada ya hapo, ni matangazo ya runinga ambayo hurushwa moja kwa moja na hapa tunaona, Ligi Kuu Bara tayari ina mdhamini ambaye ni Azam TV.

Haya yote ili yafanyike, ni lazima kuwe na mpangilio mzuri na utendaji uliotukuka badala ya yale mambo ya ujanjaujanja kama ilivyozoeleka katika mpira wetu.

Pamoja na hivyo, wadhamini ni sehemu ya wale ambao wanapaswa kupewa kipaumbele katika masuala kama haya na unaona klabu kubwa zinazopambana au kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara, zina wadhamini ambao wanasaidia mambo mengi sana.

Mfano Simba na Yanga kwa mwaka sasa wanapokea zaidi ya Sh bilioni moja kutoka kwa wadhamini wao SportPesa. Ingawa wana wadhamini wengine lakini wadhamini hawa wameandika rekodi kubwa ya kutoa fedha nyingi zaidi.

SOMA NA HII  POLISI TANZANIA YAIPIGIA HESABU SIMBA

Tumeona juzi wameingia tena mkataba na Namungo FC wakiwapa Sh milioni 120, si hapa kwao kuliko wale ambao hawajapata kabisa na hii inaifanya Namungo kuendelea kuwa na nguvu.

Wako wadhamini wengi ambao wameamua kujitosa katika kudhamini klabu za Ligi Kuu Bara na hakuna ubishi, sote tunajua kama wadhamini wameingia katika klabu fulani wanachotaka ni kuona wanajitangaza ili kusaidia kuinua mauzo ya bidhaa zao.

Klabu zinazodhaminiwa wakati fulani zimekuwa zikijisahau sana na kupata hisia kwamba udhamini ni kama zenyewe zinawasaidia wale ambao wamejitokeza kujitangaza kupitia wao.

Hii inatokana na klabu kujiona ni kubwa au maarufu kuliko wadhamini wao au wadhamini kuamua kujitangaza kupitia wao, wana shida sana. Hili limekuwa kosa kubwa sana ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi sasa.

Wadhamini ni wadau wakubwa wa maendeleo ya soka nchini na wamekuwa wakiufanya mchezo wa soka kupiga hatua kubwa sana kwa kuwa wanaingiza fedha zao.

Muhimu sana kama klabu zitaandaa utaratibu hata wa kuwapa matangazo mengi zaidi yale waliyokubaliana ili kuwafanya waamini wanapata ikiwezekana zaidi ya kile walichokubaliana.

Kuendelea kuwa na wadhamini wengi ni kuufanya mpira kuendelea kuibuka na baadaye kuifanya Tanzania kuwa na klabu nyingi bora na ligi kuu bora zaidi ndani ya Bara la Afrika.