Home Simba SC SIMBA WAMEPAA NA VISIT TANZANIA NA WENGINE WAIGE

SIMBA WAMEPAA NA VISIT TANZANIA NA WENGINE WAIGE

 


MIEZI kadhaa iliyopita, mwishoni mwaka jana, gazeti la Championi liliibua mjadala kuhusiana na Klabu ya Simba kucheza ikiwa kifua bila wadhamini wakati wa hatua za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tulitafsiri hiyo ni kama hasara na walilazimika kufanya hivyo kwa kuwa wadhamini wao SportPesa ni kampuni ya kamari kama wale wanaowadhamini Caf. Hivyo, Simba wamekuwa wakicheza mechi zao za hatua hiyo bila ya mdhamini, “plain chest”.

Ushauri wetu ulikuwa ni kuwashauri pande zote mbili kwa maana ya Simba na Serikali ya Tanzania, kuangalia namna ambavyo Simba wangeweza kuutangaza utalii.

Sitaki kusema Simba walisoma ndio wakafanya hivyo, najaribu kuelezea ilivyokuwa na pia kuzipongeza pande zote mbili za Simba na Serikali, kufikia mwafaka kwa kuliona jambo hili linafaa.

Kama Simba walikuwa wa kwanza kwenda Serikalini ni jambo la kupongezwa lakini vizuri zaidi ni kumpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro kulikubali wazo la Simba.

Nakumbuka, ilikuwa kazi ngumu sana kufikisha ushauri huo wakati wa waziri aliyepita. Ni mwanamichezo lakini huenda halikuwa analiona lina nafasi lakini Dk Ndumbaro ambaye ni mwanamichezo pia, amefikishiwa mara moja, amelichukua na kazi imefanyika.

Unaona namna ambavyo Simba wamelifanya hili jambo kwamba sasa katika mechi zao tatu za hatua ya makundi, nchi yetu itajitangaza katika nchi tatu tofauti.

Hizi ni palepale itakapocheza kwa maana ya DR Congo, Sudan na Misri. Unaona aina ya maisha ya nchi zote tatu na kwetu ni tofauti na kuna nafasi ya kushawishi watu kutembelea nchi yetu.

Sudan na Misri ni jangwa, wangehitaji kufika nchi kama Tanzania yenye hali ya hewa tofauti na wakajionea mambo kadha wa kadha. Kwa DR Congo, wana mapori makubwa lakini hawana mbuga na hifadhi kama zetu, funwe nzuri na za kuvutia kama zetu. Wako wanaoweza kushawishika.

Achana na hivyo, mechi zote za Simba kwa maana ya zile za ugenini na hapa nyumbani, zitaonekana kwenye runinga. Maana yake, Visit Tanzania itapeperuka kwa upana mkubwa na nchi yetu itajitangaza sana.

Wazo la Gazeti la Championi, lilikuwa tofauti kidogo. Sisi tulifikiri Visit Ngorongoro, Visit Serengeti, Visit Mikumi na kadhalika ingekuwa poa zaidi ili kufanya watu wajiulize maswali kuwa hayo maeneo ni wapi na wakianza kuelezewa, basi wavutiwe kufika.

Hapa kama taifa tunakwenda kuwa na faida mara mbili, achana na kuwa na timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika lakini tumepata nafasi ya kujitangaza kama Watanzania kwa kuwa nchi yetu ina mambo mengi sana ambayo watu wanayahitaji lakini hatujapata nafasi tu ya kujitangaza vya kutosha.

Dk Ndumbaro ameanza na mguu mzuri na kwa kuwa ni mwanamichezo, unaona wanamichezo wanakwenda kumuunga mkono kwa nguvu ambalo ni jambo jema sana.

Wakati Simba wameonyesha njia, Yanga wako wapi? Azam FC na wengine mpo? Lakini baada ya hapo, Serikali imeona jambo la kuliendeleza?

Maana timu zinaweza kuendelea kujitokea lakini bado Serikali nayo inaweza kutenga bajeti kidogo kuendeleza hili la kutangaza utalii wetu kupitia michezo ambayo ina nguvu na inafika sehemu kubwa ya dunia.

Mashabiki watakaonunua jezi ya Simba sasa wataonekana sehemu mbalimbali duniani na kuendelea kuitangaza nchi yetu lakini tangazo la jezi, litaendelea kudumu kwa muda mrefu sana.

Tukubaliane, mafanikio ya hili ni nchi na si shabiki wa klabu au timu fulani. Ndio maana nazishauri na klabu nyingine bila ya kuwa na ile haya kwamba wameiga, wajitokeze na kuendeleza matangazo. Serikali isimame na kuendeleza ubunifu huu hata kama ni kwa gharama nafuu.

Kimataifa, Namungo wapo, hata begani tu wanaweza kuendeleza hili. Lakini kwa kuhamasisha utalii wa ndani, basi klabu pia zinaweza kutangaza maeneo ya utalii mfano Visit Ruaha, Visit Burigi, Visit Serengeti na kadhalika.
SOMA NA HII  SIMBA vs AL AHLY...MECHI YA PESA TUPU.....TIMU ZOTE ZINATHAMANI YA BIL 100 NA ZAIDI...