Home Ligi Kuu UBABEUBABE NDANI YA UWANJA UWEKWE KANDO, MPIRA BURUDANI

UBABEUBABE NDANI YA UWANJA UWEKWE KANDO, MPIRA BURUDANI


 NAONA taratibu ndani ya uwanja kwa wachezaji ule utamaduni wa kulindana ndani ya uwanja unayeyuka kadri siku zinavyokwenda.

Hali hii ni mbaya ikiwa itaendelea kwa kuwa hakuna mchezaji ambaye anaonekana kujali hali ya mchezaji mwenzake ndani ya uwanja.

Imekuwa kawaida kwenye Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili mpaka Ligi Kuu Bara kushuhudia wachezaji wakiendelea kupambana huku mchezaji mmoja akiwa chini na hakuna anayejali.

Ila kinachonifurahisha ni kwamba pale mchezaji wa timu ambayo inamiliki mpira akiwa chini na timu yenyewe ipo kwenye umiliki hakuna anayeomba ‘fair play’ ila pale watakapopokwa mpira tu utaona wachezaji waliokuwa wanamiliki mpira wanaomba ‘fair play’.

Weka kando hiyo hebu fikiria namna ambavyo kwenye mechi za hivi karibuni kumekuwa na viwiko njenje kwa wachezaji huku maisha yakiendelea kama kawaida.

Kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara wakati Simba ikishinda bao 1-0 ilionekana kwamba Perfect Chikwende alimnyoosha kwa kiwiko mchezaji wa Biashara United, maisha yakaendelea.

Rudi nyuma pia pale Uwanja wa Nelson Mandela, Bernard Morrison alikutana na balaa la Salum Kimenya na usisahau kwamba huyohuyo Morisson Uwanja wa Uhuru alionekana kupigana na nahodha wa Ruvu Shooting, Juma Nyoso.


Labda utakuwa umesahau kwamba Luis Miquissone alichezewa faulo isiyo salama na Kibwana Shomari kwa kweli hali sio nzuri kwa sasa kwa wachezaji wetu.

Twende pale Azam Complex, kumbuka kuwa kwa sasa Yahya Zayd atakuwa nje kwa muda wa wiki sita na alichezewa faulo ndani ya uwanja akiwa kwenye mapambano mbele ya Mbeya City.

Pia Prince Dube naye kwenye mchezo huo dhidi ya Mbeya City akiwa hayupo kwenye hatari yoyote ile kwa kuwa alikuwa ameotea bado alikutana na ngumi kutoka kutoka kwa mchezaji wa Mbeya City.

Yaani ni mwendo wa ubabeubabe ndani ya uwanja katika dakika 90 za kusaka ushindi.

Pia wakati Azam FC wakisaka pointi tatu mbele ya Tanzania Prisons kwenye sare ya bila kufungana bado nguvu nyingi zimekuwa zikitumika.

SOMA NA HII  KOCHA BARAZA WA BIASHARA UNITED AMTAKA BANDA KIKOSINI

Nakumbuka kuna faulo moja alicheza mkongwe Agrey Morris na kuonyeshwa kadi ya njano mpaka yeye alionekana akijutia namna alivyofanya kwa kuwa anatambua kwamba majeraha ni maumivu makubwa kwa mchezaji.

Mbali na hilo pia kipa wa Azam FC, Mathias Kigonya naye alionekana akimpiga kiwiko mchezaji wa Tanzania Prisons hivyo hata Prisons nao walionekana wakitumia nguvu nyingi.

Wachezaji ni muhimu kujali afya za wachezaji wenzenu kwani kuumizana kwa hasira hii sio sawa na kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa mchezaji mwenzake.

Sio Ihefu pekee, iwe Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Lipuli, Njombe Mji mpaka Namungo ni muhimu kulindana ndani ya uwanja.

Dakika 90 isiwe vita bali iwe ni burudani na furaha kama asemavyo Mecky Maxime wa Kagera Sugar.