Home Simba SC WACHEZAJI SIMBA SC WAPEWA DOLA 5,000 KILA MMOJA KWA KUIFUNGA AS...

WACHEZAJI SIMBA SC WAPEWA DOLA 5,000 KILA MMOJA KWA KUIFUNGA AS VITA


BAO pekee la ushindi lililofungwa na straika hatari wa Simba, Chriss Mugalu limewapa neema nyota 27 wa kikosi hicho, waliowasili jana kutoka Kinshasa, DR Congo walipoenda kucheza mechi dhidi ya AS Vita baada ya mabosi wao kulitathmini na kulipa thamani ya Sh200 milioni.

Simba ilipata ushindi huo wa 1-0 katika mchezo huo wa kwanza wa Kundi A kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Mugalu na kuipa Simba alama tatu na kuongoza kundi hilo lenye Al Ahly ya Misri na Al Merreikh ya Sudan na kuwapagawisha mabosi wa klabu hiyo walioambatana na timu hiyo.

Mwanaspoti lililokuwa bega kwa bega na Simba jijini humo, lilidokezwa kuwa, kabla ya mchezo huo nyota wa Simba waliahidiwa pesa ambayo haikutajwa, lakini mara baada ya ushindi kupatikana wakaambiwa watapewa Sh200 milioni kama bonansi nje ya mishahara yao.

Pesa hiyo itagawanywa kwa wachezaji wote 27 waliosafiri na kikosi hicho hadi Kinshasa, lakini mkwanja huo utagawanywa katika mafungu matatu.

Wachezaji wote waliocheza hata dakika moja kila mmoja atapata si chini ya Sh10 milioni ambazo ni sawa na (dola) $5,000 wakati waliokuwa benchi, inaelezwa watapewa si chini ya Sh5 milioni na ambao hawakucheza kabisa watapata chini ya hapo.

Baada ya kupatikana ushindi huo wachezaji wa Simba baada ya kufahamu watavuta mkwanja huo mrefu kuanzia uwanjani, kambini hata safarini walikuwa na furaha ya mara kwa mara.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alipoulizwa na Mwanaspoti alikiri wamewekeza katika kuhakikisha timu yao inafanya vizuri katika mashindano hayo msimu huu na kufika mbali kama malengo yao yalivyo.

Barbara alisema hawezi kueleza kiasi gani watawapatia wachezaji kama motisha baada ya ushindi lakini ni pesa nyingi ambayo wataifurahia.

“Ukiachana na motisha hiyo tumewekeza katika teknolojia ili kuona wachezaji na benchi la ufundi wanapata muda wa kuwasoma wapinzani wetu kabla ya kwenda kukutana nao,” alisema Barbara na kuongeza;

“Jukumu langu ni kuhakikisha nawasaidia na kuwapa benchi la ufundi ushirikiano ili waweze kufanya vizuri katika kila mashindano.”

SOMA NA HII  SIMBA YAWAPIGIA MAGOTI WA TZ WANAOISHI SAUZI....WAOMBA NGUVU YA KUUJAZA UWANJA WA ORLANDO ....

MSIKIE LWANGA

Kiungo mkabaji wa Simba, Taddeo Lwanga akizungumzia juu ya bonasi hiyo alisema sio Simba bali ni timu nyingi za Afrika kumekuwa na tabia hiyo ya kuweka motisha ya posho ili wachezaji kwenda kwenda kupambana zaidi.

Lwanga alisema katika mashindano haya kuna zawadi inatoka kwa Shirikisho la soka Afrika (CAF), ili kuweza kuwa na kipato cha kutosha kwa kila timu kuweza kujiandaa.

“Wakati CAF, wakiwa wanatoa pesa hiyo nasi viongozi huwa wanatuwekea motisha mbalimbali kama hizi ili kufikia yale malengo ambayo mmejiwekea. Katika kila hatua mnayozidi kwenda pesa hiyo kutoka CAF, nayo anazidi kuongezeka lakini hata wadhamini nao hufikilia kuweza kwenye timu ambazo zinafanya vizuri katika mashindano haya,” alisema Lwanga raia wa Uganda.