WAKIWA Uwanja wa Mkapa, mabingwa watetezi, Simba leo wamechezewa pira gwaride na kikosi cha Tanzania Prisons na kuwafanya wafanye msako mkali kutafuta bao la kufutia machozi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Kipindi cha kwanza dakika ya 23, Chris Mugalu akiwa na kipa Jeremia Kisubi alipiga penalti iliyookolewa na kipa huyo wa Tanzania Prisons ambaye leo alikuwa kwenye ubora wake dakika zote 90 mpaka ubao ukasoma Simba 1-1 Tanzania Prisons.
Ni Salum Kimenya, kiraka wa Tanzania Prisons alianza kumtungua Aishi Manula dakika ya 56 kwa faulo aliyopiga nje kidogo ya 18 na ikapenya kwenye ukuta wa Simba na kumpoteza kipa namba moja Aishi Manula.
Baada ya bao hilo Didier Gomes alikuwa haamini anachokiona kwa kuwa vijana wa Prisons walikazana kucheza lile pira gwaride ambalo liliwafanya Simba wakazane kusaka ushindi huku mipango yao ikidhibitiwa.
Licha ya kwamba Prisons walikuwa 10 uwanjani baada ya Jumanne Elifadhil kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea faulo Mzamiru Yassin bado mambo yalikuwa mazito kwa Simba.
Mpaka dakika 90 zinakamilika ubao ulikuwa unasoma Simba 0-1 Prisons jambo lililowafanya Prisons waamini watasepa na pointi tatu nyingine kama walivyowatungua bao 1-0 Uwanja wa Nelson Mandela.
Katika dakika 5 za nyongeza zikiwa zinafika tamati, Luis Miquissone alimalizia pasi ya kichwa ya Bernar Morrison na kufanya ubao usome Simba 1-1 Prisons.
Sare hiyo inawafanya Simba wafikishe jumla ya pointi 46 wakiwa wamecheza mechi 20 huku wapinzani wao Yanga wakibaki kileleni na pointi zao 50 tofauti ya pointi 4.
Prisons wanafikisha jumla ya pointi 28 na wanapanda kutoka nafasi ya 10 mpaka ya 9.