USHINDI wa 3-0 waliopata Simba dhidi ya Al Merrikh unawafanya Simba kufikisha pointi 10 na kuwafanya wasubiri pointi moja tu ili kujihakikishia nafasi ya kwenda hatua ya robo fainali.
Kusubili kwa pointi moja kunatokana na mtu wa pili katika kundi A ambaye ni Al Ahly kuwa na pointi saba huku nafasi ya tatu ikishikiliwa na AS Vita wenye pointi nne na Merrikh wakiwa na pointi moja.
Kwa maana hiyo zikiwa zimebaki mechi mbili, Simba anahitaji pointi moja tu katika mchezo ujao dhidi ya As Vita na kufikisha pointi 11 akijihakikishia kuongoza kundi A.
Wakati huo Al Ahly wao wakiwa ugenini dhidi ya Al Merrikh hata wakishinda watakuwa na pointi 10 na kuwafanywa washike nafasi ya pili.
Katika mchezo wa Simba dhidi ya Merrikh Kwenye kipindi cha kwanza Simba walionekana kuweza kumiliki mpira huku wakicheza kwa kushambulia wakionyesha kabisa kuhitaji bao la mapema.
Mawinga wa Simba, Luis Miquissone na Benard Morrison walionekana kupeleka mashambulizi mara kwa mara langoni mwa El Merrikh na ilikuwa ikiwapa presha.
Dakika 19 Luis Miquissone aliifungia Simba bao la kwanza baada ya kupokea pasi kutoka kwa Clatous Chama akiwa ndani ya boksi na yeye akaupiga mpira ukaenda moja kwa moja wavuni.
Dakika 30 Simba walikosa goli la pili baada ya winga, Benard Morrison kupiga pasi kwa Chris Mugalu akiwa katikati ya mabeki ndani ya boksi lakini wakati anaunganisha aligusa vibaya mpira na kutoka kwa juu.
Dakika 37 kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin alikosa goli la wazi baada ya kukosa utulivu alipopigiwa pasi na Chama, Mzamiru alishindwa kutulia badala yake alipiga shuti na mpira kutoka nje.
Dakika 40 Simba ilipata bao la pili baada ya Benard Morrison kupiga pasi ndefu akiwa katikati ya uwanja na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliuwahi mpira huo na kumuangalia kipa wa El Merikkh na kupiga shuti dogo lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Katika kipindi cha pili dakika 45 Simba walifanya mabadiliko ya kutoka Mzamiru Yassin na kuingia Lary Bwalya, huku Merikkh akiingia Ahmed Yusuph akitoka, mabadiliko hayo yakiwa kwenda kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
Dakika 50 Mugalu alionyesha umahili mkubwa akiwa ndani ya dimba baada ya kupokea pasi ya krosi iliyochongwa vizuri na Luis Miquissone na yeye aliutuliza na kufyatuka shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Goli hilo halikuonekana kuwavuruga El Merikkh lakini kila walipokuwa wanajaribu kuipenya safu ya ulinzi Simba walikuwa wanaishia njiani.
Dakika 66 Wagdi Alla wa Merikkh alionyeshewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi kiungo wa Simba, Tadeo Lwanga kwa kumnyanyulia mguu.
Dakika 68 kiungo wa Merrikh, Mohamed Abbas alipiga shuti kali nje ya boksi lakini mpira ulitoka nje ya goli.
Simba walifanya mabadiliko mengine dakika 71 kuwatoa Benard Morrison na Chris Mugalu huku nafasi zao zikichukuliwa na Jonas Mkude na Meddie Kagere.
Merikkh walitaka kupata bao la kufutia machozi dakika 81 kupitia kwa Darren Mattocks lakini Manula aliucheza na kuwa kona isiyokuwa na faida
Simba walifanya mabadiliko mengine dakika 83 kwa kumtoa Luis Miquissone na kuingia Francis Kahata, mabadiliko ambayo yalionekana kama vile ni ya kimbinu katika kuchelewesha mpira.