WATANZANIA kwa sasa wanaendelea kutazama uhondo wa michuano ya kimataifa ile ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na kuwa na timu mbili katika michuano hiyo ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Tanzania inawakilishwa na Simba ambao wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na jana Jumanne walikuwa na mechi ya hatua ya makundi walipokuwa wanacheza na Wasudan Al Merrikh ukiwa mchezo wa marudiano baina ya timu hizo baada ya ule wa kwanza kule Sudan.
Dakika 90 zilikamilika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kuwafanya wabaki na pointi tatu kisha wamefikisha jumla ya pointi 10 wakiwa ni namba moja kwenye kundi A.
Lakini kwenye Kombe la Shirikisho, Tanzania wana wawakilishi ambao ni Namungo. Klabu hiyo nayo ipo hatua ya makundi ya kombe hilo ambapo wao wana kibarua leo Jumatano dhidi ya Pyramids ya Misri.
Huu ni mchezo wa pili kwa Namungo wanaotokea Lindi baada ya kupoteza mbele ya Raja Casablanca mapema wiki iliyopita kwa bao 1-0. Japo walifungwa lakini Namungo wana nafasi ya kurekebisha makosa na kupita kwenye hatua hii ya makundi ambayo wapo kwa sasa.
Wakati leo Jumatano wanapambana na Pyramids kuna kitu nataka kuwakumbusha Namungo ambacho kinaweza kuwa faida kwao hasa katika nafasi ya kusonga mbele katika hatua hiyo ya makundi.
Kitu ambacho wanatakiwa kukichukua na kukifanyia kazi wauaji hawa wa Kusini ni kupita kwenye njia ambayo iliwapa mafanikio Simba kwa msimu wa 2018/19 ya kufanya vizuri wakiwa nyumbani.
Tayari wameshapoteza pointi tatu katika mechi yao ugenini kule Morocco lakini wanachotakiwa kukifanya Namungo leo ni kutokukubali kupoteza pointi lakini hata kwenye mechi zao mbili zaidi ambazo watacheza nyumbani.
Hali hiyo itawasaidia kwa sababu watakuwa na uhakika wa kukusanya pointi tisa wakiwa nyumbani ambazo kwa msimu wa 2018/19 ndizo ziliwabeba Simba na kutinga hatua ya robo fainali ambapo walikutana na TP Mazembe.
Kwenye michuano hii ni ngumu sana kupata pointi unapokuwa ugenini kutokana na mazingira ya soka lenyewe la Kiafrika lakini Namungo wanatakiwa kutumia ile faida ya kucheza wakiwa nyumbani na kubeba pointi zote katika michuano hii.
Kwa sasa hesabu za Namungo zinatakiwa kuanza kuchukua pointi kwa Pyramids leo Jumatano kwa ajili ya kuanza kusafisha njia ya kufika robo fainali lakini baada ya hapo ni kwenye mechi mbili zijazo dhidi ya Raja na Nkana FC.
Hesabu za kuweka akilini kwamba Namungo wanaweza kuchukua pointi wakiwa ugenini hasa katika hatua hii nafikiri kwanza ziwekwe kando licha ya kwamba timu yoyote inaweza kupata matokeo katika mazingira yoyote ile. Nasema kuchukua pointi ugenini kutawapoteza Namungo kwa sababu ya wapinzani ambao wamepangwa nao kuwa wataalamu wa kumaliza shughuli kila wanapocheza nyumbani kwao.
Kwa wakati huu nawasihi sana Namungo kufikiria sana namna ya kusaka pointi nyumbani ambazo zitawapa uhakika wa kufika mbali wanapopataka kuliko kufikiri wanaweza kushinda na ugenini. Lengo la kwanza liwe kushinda nyumbani kisha ikitokea ugenini basi iwe ziada.
Kiufupi tu Namungo wanaweza kuitazama njia ambayo waliamua kupita Simba kwa msimu wa 2018/19 kwa ajili ya kufika hatua za mbali katika kombe hilo wanaloshiriki.