NYOTA ya mshambuliaji wa Simba, Luis Miquissone imeendelea kung’aa baada ya kuchaguliwa kwa mara nyingine kwenye kikosi bora cha wiki cha raundi ya nne ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwazidi kete wachezaji mastaa wa TP Mazembe ambao hata mmoja wapo ameshindwa kuwemo katika kikosi hicho.
Kiwango bora kilichoonyeshwa na Miquissone katika mchezo wa raundi ya nne ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh, Jumanne iliyopita ambapo alihusika na mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0 ambao Simba iliupata katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam kilimfanya mshambuliaji huyo kutoka Msumbiji kupigiwa kura zilizomuingiza katika kikosi hicho.
Katika mchezo huo, Miquissone alifunga bao moja na kupika lingine na kuifanya Simba iibuka na ushindi huo mnono ambao umeifanya ifikishe jumla ya pointi 10 na kuongoza msimamo wa kundi A mbele ya Al Ahly, AS Vita Club na Al Merrikh.
Hiyo ni mara ya pili kwa Miquissone kuingia katika kikosi bora cha wiki katika hatua hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwani mara ya kwanza ilikuwa ni baada ya mechi ya raundi ya pili dhidi ya Al Ahly ambapo pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa wiki na mfungaji wa bao bora.
Lakini safari hii haikuishia kwa Miquissone tu bali pia hata beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ naye alichaguliwa kuwemo katika kikosi hicho bora cha raundi ya nne baada ya kufunga moja kati ya mabao ya Simba katika ushindi wake nyumbani dhidi ya Al Merrikh.
Wakati Simba ikitoa wachezaji wawili katika kikosi hicho, Mamelodi Sundowns inaongoza kwa kutoa wachezaji watatu, Al Ahly ikiwa na wawili kama ilivyo kwa Simba na MC Alger wakati huo timu za Esperance na Pero Luanda kila moja ikitoa mchezaji mmoja.
Kikosi bora cha wiki cha raundi ya nne ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kinaundwa na kipa Denis Onyango (Mamelodi) wakati mabeki ni Diogenes Joao (Petro Luanda), Mouad Haddad (MC Alger), Mosa Lebusa (Mamelodi) na Tshabalala (Simba)
Viungo ni Meldi Benaldjia (MC Alger), Yasser Ibrahim (Al Ahly) na Lebohang Maboe (Mamelodi) wakati washambuliaji ni Miquissone (Simba), Hamdouni Elhouni (Esperance) na Mohamed Magdi Afsha (Al Ahly)