VIVIER Bahati, kocha msaidizi wa Azam FC amesema kuwa kupitia makosa ambayo yanafanywa na wapinzani wao inazidi kuwaongezea nguvu ya kufanya vizuri kwenye mechi zao zilizobaki jambo litakalowarejesha kwenye kasi yao ya awali.
Azam FC ambayo ipo chini ya Kocha Mkuu, George Lwandamina ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo imekusanya pointi 44 baada ya kucheza mechi 24.
Kinara Yanga mwenye pointi 50 aliyumba ndani ya mechi zake sita za mzunguko wa pili na alipoteza mchezo wa kwanza kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union pale Mkwakwani, Tanga.
Simba ambao ni mabingwa watetezi wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 46 baada ya kucheza mechi 20, Tanzania Prisons waliwapa tabu Uwanja wa Mkapa kwa kuwachezesha pira gwaride na kuwafanya wagawane pointi mojamoja kwenye sare ya kufungana bao 1-1.
Bahati amesema:”Kupitia makosa ya wapinzani wetu inazidi kutupa nguvu ya kufanya vizuri na ikiwa tutashinda mechi ambazo tutacheza basi tutarejea kwenye kasi yetu ile ambayo tulianza nayo.
“Ushindani ni mkubwa na kila mmoja anatambua kwamba kupata ushindi ni kitu cha msingi, mashabiki wazidi kutupa sapoti,” .