KWENYE hatua ya makundi ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi cha Simba kimeonekana kuwa na ubabe kwa kuwa kila kinapopata nafasi ya kuwakilisha nchi, wachezaji wamekuwa wakipambana.
Simba imekuwa na mwendo mzuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, na kiwango chao bora kimewafanya kuweka rekodi saba ambazo ni hizi hapa
UBABE WA SIMBA AFRIKA MASHARIKI
Simba imetinga hatua ya makundi ya michuano ya Afrika mara sita ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni msimu wa 1974 na msimu huu ilifika mpaka hatua ya nusu fainali, 1993 ikafika fainali ya Kombe la Shirikisho ikafungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast, 1994 ikafika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.
2003 ilifika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, kisha 2018-19 ikatinga hadi robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, halafu mwaka huu imetinga hatua ya makundi ikiwa tayari imetanguliza mguu mmoja robo fainali.
Simba ndiyo timu ya Afrika Mashariki inayoongoza kwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Afrika mara nyingi zaidi.
KUTOKUFUNGWA
Katika misimu sita ambayo Simba wametinga makundi, msimu huu ndiyo wana rekodi bora zaidi za kiulizi baada ya hadi sasa kucheza mechi nne za hatua ya makundi bila kufungwa bao lolote.
Hayo ni maendeleo makubwa ukilinganisha na mara ya mwisho kwa Simba kutinga hatua ya makundi msimu wa 2018-19 waliporuhusu mabao 10 katika mechi nne za mwanzo.
YAIFUNIKA YANGA
Wakati Simba ikiwa imetinga hatua ya makundi ya michuano ya Afrika mara sita, mahasimu wao Yanga wameingia mara tano msimu wa 1969 walipofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, 1970 waliporudia mafanikio ya robo fainali ya michuano hiyo, 1998 ilipofika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na kumaliza nafasi ya mwisho, 2016 na 2018 walipofika hatua ya makundi Kombe la Shirikisho wakiwa chini ya kocha Hans Pluijm na George Lwandamina, mtawalia
KIKOSI BORA CHA CAF
Kwa msimu huu wa 2021 Simba imeonyesha ubabe kwa kutoa jumla ya wachezaji wanne kwenye kikosi bora cha wiki ndani ya Caf, jambo ambalo halijawahi kufanywa na timu yoyote Afrika Mashariki.Kikosi cha kwanza kiliwatoa nyota wawili ambao ni Luis Miquissone na Joash Onyango na kile cha pili kilitoka na majina ya Mohamed Hussein na Luis.
Pia msimu huu, Luis bao lake dhidi ya Al Ahly linatajwa kuwa bora katika mechi za raundi ya pili ya makundi, alifunga akiwa nje ya 18, Uwanja wa Mkapa.
KUWAKALISHA WAARABU MARA MBILI
Waarabu wa Misri, Al Ahly wanaijua chungu ya Simba kwa kuwa waliambulia kipigo mara mbili Uwanja wa Mkapa, hakuna timu ya Afrika mashariki iliyowahi kuwafunga mabingwa hao wa Afrika mara mbili.
Msimu wa 2018/19 walikalishwa Uwanja wa Mkapa kwa bao 1-0 na mara ya pili ni 2020/21 Uwanja wa Mkapa kwa bao 1-0, zote ilikuwa ni hatua ya makundi.Yanga imeshawahi kuifunga Al Ahly mara moja tu, ilikuwa Machi 2014 kwenye raundi ya kwanza iliposhinda kwa bao 1-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
ZIGO LA MABAO KIMATAIFA
Ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Patrick Aussems, 2018/19 Simba iliweka rekodi ya kubebeshwa zigo la mabao ya kutosha ila rekodi hiyo ilishindwa kuivunja ile ya Yanga kufungwa mabao 19 hatua ya makundi mwaka 1998.
Simba baada ya kucheza jumla ya mechi 6, safu yake ya ushambuliaji ilifunga mabao 6 na ile ya ulinzi iliokota jumla ya mabao 13, Yanga ilipotinga hatua ya makundi msimu wa 1998 ilicheza mechi 6, safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 5 na ilifungwa jumla ya mabao 19.
KIBOKO YA VIGOGO WA AFRIKA
Zamalek walisanda mbele ya Simba, ilishinda kwa penalti 3-2 msimu wa 2003 katika Ligi ya Mabingwa baada ya dakika 90 kutoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 na iliwavua ubingwa ambao waliutwaa msimu wa 2002.
Al Ahly ya Misri pia imekuwa ikipata tabu kupata ushindi Uwanja wa Mkapa kwa kuwa Simba imeshinda mara mbili kwenye hatua ya makundi na msimu huu imewafunga wakiwa ni mabingwa watetezi.