TIMU ya Namungo FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Hemed Morocco imeanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao wa tatu, wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Nkana ya Zambia utakaopigwa Ijumaa ya Aprili 2, Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Namungo imeanza kwa kupoteza mechi zake mbili za hatua ya makundi ambapo ya kwanza ilipoteza ugenini, kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Raja Casablanca na ile ya pili Uwanja wa Mkapa ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Pyramids Uwanja wa Mkapa.
Kwenye kundi D ikiwa imecheza mechi mbili haijaambulia pointi kibindoni na ina kazi ya kukutana na Nkana FC ya Zambia.
Pyramis na Raja Casablanca zinaongoza kundi na pointi zao ni sita kwa kuwa hawajapoteza mechi zao mbili huku Nkana na Namungo zikiwa hazijaambulia ushindi kwenye mechi walizocheza.
Ofisa Habari wa Namungo FC, Kidamba Namlia amesema kuwa makosa ambayo waliyafanya mwanzo wanayafanyia kazi wana amini watapata matokeo kwenye mechi zao zijazo.
“Kushindwa kupata ushindi kwenye mechi zilizopita haina maana kwamba ni mwisho wetu kupambana na kupata matokeo chanya kwenye mechi zetu zijazo tutapata matokeo chanya.
“Ushindani ni mkubwa na kila timu inahitaji ushindi hivyo mashabiki wetu wasiwe na mashaka tupo tayari kufanya vizuri,” amesema.