BAADA ya kuzichungulia Simba na Yanga na kubaini zina viungo matata, mabosi wa Azam FC nao wameamua kushusha mkata umeme wao kutoka Zimbabwe kimyakimya.
Kule Jangwani, mashabiki wa Yanga wanatambia mido wao mkabaji Mukoko Tonombe, huku wale wa Simba wakajibu mapigo kwa kumleta Mganda Thadeo Lwanga ambaye anakaba kibabe kiasi cha kuwanyia raha wapinzani wake uwanjani, ndipo Azam nao wakaona isiwe tabu.
Ndani ya majengo ya Azam kuna kiungo mkabaji Gerald Takwara anayefanyiwa majaribio ya mwisho chini ya Kocha George Lwandamina na kama mambo yatatiki basi atasajiliwa ili kuchukua nafasi ya mtu na kwenda kuliamsha dhidi ya kina Tonombe na Lwanga.
Kocha Lwandamina mapema aliwaambia mabosi wake kwamba anataka mtu mwingine mkabaji katika kikosi hicho baada ya kuona Mnyarwanda Ally Niyonzima bado hampi anachotaka.
Takwara ni mmoja kati ya viungo bora kutoka Zimbabwe wanaojua kutimiza majukumu ya ukabaji katika kiungo ambapo Mwanaspoti linafahamu kwamba tayari Lwandamina amekaribia kupitisha usajili wake.
Hata hivyo, taarifa njema kwa Azam ni kwamba kiungo huyo atamaliza mkataba wake Juni na klabu ya Ngezi Platinum, hatua ambayo itawapa matajiri hao nafasi nzuri ya kumsainisha mkataba katika dirisha kubwa la usajili.
Takwara mapema aligoma kuongeza mkataba na Ngezi Platinum akirahisisha safari yake ya kucheza soka tena nje ya ardhi ya Zimbabwe.
Awali, Takwara aliwahi kuwa staa muhimu kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) akiichezea Ajax Cape Town kabla ya baadaye kurejea Zimbabwe.
Endapo Azam itamalizana naye watakuwa wamefanya usajili mzuri katika kuimarisha safu yao ya kiungo lakini pia watakuwa wameiongezea ulinzi ukuta wao ambao kwa sasa unasimamiwa na Yacob Mohamed anayechezeshwa kama kiungo mkabaji mbele ya kina Aggrey Morris, Abdallah Kheri au Daniel Amoah!