UONGOZI wa Azam FC umefunguka kuwa hauna mpango wa kumsajili beki wa Klabu ya Simba, Gadiel Michael kwa kuwa hakuna mapendekezo yoyote kutoka kwa kocha, George Lwandamina ya maboresho katika nafasi hiyo.
Gadiel aliyejiunga na Simba msimu uliopita wa 2019/20 akitokea Yanga amekuwa na wakati mgumu kupata nafasi ndani ya kikosi cha Simba.
Hii ni kutokana na ushindani mkubwa wa namba kutoka kwa nahodha msaidizi wa kikosi cha timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ kiasi cha hivi karibuni kuhusishwa kuwa na mpango wa kurejea Azam.
Gadiel alikulia ndani ya kikosi cha vijana cha Azam tangu mwaka 2014 kabla ya kuondoka mwaka 2017, ambapo alijiunga na Klabu ya Yanga aliyoichezea mpaka mwaka 2019.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Azam, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’ alisema: “Ndani ya kikosi chetu kocha mkuu pekee ndiye anayehusika na masuala yote ya usajili na mpaka sasa hajapendekeza usajili wa beki wa kushoto.
“Lakini pia sera yetu ya usajili inatutaka kusajili mchezaji anayecheza kwenye kikosi cha timu aliyotoka na siyo ambaye hapati nafasi.
“Mpaka sasa hatujapokea maombi yoyote rasmi kutoka kwa Gadiel, na kama amefanya hivyo basi itakuwa alimuomba kiongozi binafsi ambaye hajalifikisha suala hilo kwenye meza yetu.”