Home Makala KUELEKEA KARIAKOO DABI KESHO…MASAU BWIRE KAONA ISIWE TABU USHINDI KAUPELEKA HUKU…

KUELEKEA KARIAKOO DABI KESHO…MASAU BWIRE KAONA ISIWE TABU USHINDI KAUPELEKA HUKU…

Dabi ya Kariakoo, Yanga dhidi ya Simba itakayochezwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa pamoja na kuwa mechi ngumu, isiyotabirika, Mzee wa Mpapaso naipatia Simba asilimia 60 ya ushindi.

Mara nyingi mechi hizi za Dabi, Yanga dhidi ya mtani wake Simba huamuliwa kwa dakika 90, aliyejiandaa vizuri ndiye hupata matokeo mazuri.

Lakini wakati fulani, yule ambaye tulimuona yuko vizuri, tukawa na uhakika wa zaidi ya asilimia 70 kwamba atashinda, imekuwa ikitokea kinyume, hali ambayo inaniaminisha Mzee wa Mpapaso kusema dakika 90 zitaamua mshindi.

Dabi ya Kariakoo ni ngumu na ina mambo mengi, vimbwanga na mambo meusi hupenyezwa, huchukua nafasi kubwa, hali ambayo wengi hushindwa kuamini masuala ya ufundi na uwezo wa wachezaji kuamua mshindi.

Asilimia 60 za ushindi ninazowapatia Simba katika mchezo wa kesho ni kutokana na ufanisi na ubora wao katika siku na mechi za karibuni hasa za kimataifa zilizowapatia matokeo chanya, lakini kwa Dabi hii, hicho siyo kipimo kabisa cha ushindi. Mchezo huu huwa ni tofauti sana. Simba imefanya vizuri kimataifa dhidi ya Primier de Agosto, matokeo yaliyoiwezesha kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo kuwapa wachezaji morali na kujiamini zaidi kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Yanga.

Yanga michezo miwili ya kimataifa iliyocheza dhidi ya Al Hilal haikufanya vizuri, iliondolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa katika mzunguko tu wa kwanza, hivyo kwa kiasi fulani imewashusha morali na kuwaongezea presha.

Mchezo huo, Simba itacheza kwa kujiamini, bila presha kutokana na matokeo mazuri ya nyuma, tofauti na Yanga ambayo itacheza kwa presha ili kuwarejesha mashabiki wao katika matumaini ambayo wamelipoteza baada ya kuondolewa Ligi ya Mabingwa.

Yanga ikiingia uwanjani na kucheza kwa presha, inaweza kujikuta inaipandisha zaidi presha ya mashabiki wake kwa kuupoteza mchezo huo dhidi ya Simba.

Wanachopaswa kukifanya wachezaji wa klabu hiyo ya Jangwani ni kutulia, kuwa makini na kucheza bila mihemko hali ambayo itawafanya wacheze mchezo mzuri, wenye kuweza kuwapatia matokeo chanya.

Wakiingia uwanjani na presha za mashabiki, wakacheza kwa presha, wanaweza kujikuta wanapigwa kama ngoma ya Kisukuma, wacheza shoo wa ngoma hiyo badala ya kuicheza Kibongobongo, kwa kuchanganyikiwa wakacheza mapigo ya Lizombe!

Dabi ya Yanga na Simba, ni mechi ambayo naiona itakuwa na mabao kutokana na aina ya washambuliaji waliopo katika vikosi vya timu zote mbili, ni wachezaji wenye akili na maarifa ya kutafuta mabao.

Washambuliaji Fiston Mayele, Feisal Salum kwa upande wa Yanga, wanao uwezo wa kuamua matokeo kwa uwezo binafsi, kadhalika Clatous Chama na Moses Phiri kwa upande wa Simba.

Katika eneo la ulinzi kwa timu zote limeimarika japo kwa kiasi fulani, kwa matokeo ya mechi za karibuni, Simba wameimarika zaidi kwa kutokuruhusu mabao mengi ya kufungwa langoni mwao, tofauti na Yanga ambao wameruhusu mabao mengi kuliko Simba.

Yanga inawategemea zaidi mabeki Bakari Nondo, Kibwana Shomari na Dickson Job, Simba wao wakiwategemea zaidi Hennock Inonga, Joash Onyango na Mohammed Ouattara.

Makipa wa timu zote mbili ni mahiri, wenye uwezo mkubwa wa kudaka mikwaju, Djigui Diarra wa Yanga na Aishi Manula wa Simba ni makipa wa kuaminika katika kulilinda lango, kwa uimara wao, lazima akili kubwa ya washambuliaji itumike ili kupata mabao.

Tunatarajia mchezo wa kiungwana, uwanjani na nje ya uwanja pia ili watazamaji waweze kuburudika na kuufurahia, tofauti na hapo ni kuitia doa Dabi hiyo inayofuatiliwa na mataifa karibia yote Afrika.

Waamuzi waliopangwa kuichezesha mechi hiyo kina Ramadhan Kayoko kutoka Dar es Salaam na ‘Line One’ ni Mohammed Mtono wa Tanga huku ‘Line Two’ akiwa Janeth Balama wa Iringa. Hawa wanatakiwa kuzingatia sheria, wazitafsiri vilivyo, wasijiingize kwenye presha, ushabiki na ushawishi wa aina yoyote kwa malengo ya kupuliza na kung’ata katika maamuzi yao, wasimame katika kweli, usawa na haki.

Mechi ya kesho ipo kwenye msawazo, mzani umekaa sawa, mjanja tu, atakayeitumia vema nafasi atakayoipata, itaibuka mshindi.

Mzee wa Mpapaso pamoja na kuwatakia mchezo mwema watani hao, niwakumbushe tu wadau kwamba, mechi ya Yanga na Simba, huamliwa na dakika 90.

SOMA NA HII  TETESI ZA USAJILI ULAYA: CHEALSEA WAIVIMBIA BARCELONA KWA AUBAMEYANG...WAKATAA KUTOA MZIGO WOTE...