Home CAF KOCHA AL MERRIKH : RUSHWA KWA WAAMUZI IMETAWALA MECHI ZA KLABU BINGWA

KOCHA AL MERRIKH : RUSHWA KWA WAAMUZI IMETAWALA MECHI ZA KLABU BINGWA


Kocha wa zamani wa Al Merrikh ya Sudani ambapo sasa ni kocha Mkuu wa  Al-Ittihad ya Libya, Diego Garzitto amedai mashindano ya klabu yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), yamegubikwa na vitendo viovu vya rushwa kwa marefa ambavyo ndivyo vinaamua timu za kutwaa ubingwa na sio ubora na uwezo wa uwanjani.

Kocha huyo ameenda mbali zaidi kwa kuitaja timu ya TP Mazembe kama kinara wa kutoa rushwa kwa waamuzi ili waibebe jambo ambalo linaondoa maana halisi ya ushindani.

Akinukuliwa na mtandao wa www.mysoccer24.com mara baada ya mahojiano yake na kituo cha luninga cha Al Wasat cha Libya, Garzitto alisema kuwa nchi nyingi Afrika, viongozi wa klabu wamekuwa wakitumia nguvu kubwa nje ya uwanja hasa kuwahonga marefa na wale wanaowapa kiasi kikubwa cha fedha ndio hufanikiwa

“Bila shaka kuna uongozi ambao unajua kushughulika na mashindano ya klabu ya Caf kwa mfano TP Mazembe wako karibu sana na marefa. Namaanisha kushindana ni lazima uwe angalau na marefa wawili au watatu katika mfuko wako,” alisema Garzitto.

Garzitto ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika kutokana na kuwahi kufundisha idadi kubwa ya timu ikiwemo TP Mazembe ambayo mwaka 2009 aliiongoza kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mbali na TP Mazembe na Al Ittihad, timu nyingine za Afrika ambazo Garzitto amewahi kuzifundisha ni Wydad Casablanca, Al Hila Omdurman, CS Constantine, Al Merrikh, timu ya Taifa ya Togo na timu ya taifa ya Ethiopia.

Hii sio mara ya kwanza kwa klabu za Afrika kuhusishwa na rushwa kwa waamuzi ili wazisaidie zifanye vizuri katika mechi zao za mashindano ya klabu Afrika.

Mwaka 2018, refa Norman Matemera wa Zimbabwe aliwasilisha ushahidi wa kuhongwa kiasi cha Dola 30,00 yeye na wasaidizi wake kutoka timu ya Deportivo Niefang ya Guinea ya Ikweta ili awabebe katika mechi yao nyumbani dhidi ya Williamsville ya Ivory Coast baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 2-0 ugenini.

SOMA NA HII  WAPINZANI WA SIMBA CAF WAFANYA KUFRU....WAMFUNGA MTU GOLI 15-1...ALAFU HAWARINGI WALA NINI...