Home Simba SC KOCHA MKUU WA SIMBA AWEKA REKODI YAKE

KOCHA MKUU WA SIMBA AWEKA REKODI YAKE


 BAADA ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo uliopigwa, Jumatatu, Uwanja wa Mkapa Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, ameweka rekodi ya kutopoteza mchezo kwenye mashindano yote kwa dakika 810, tangu ajiunge na kikosi hicho.

Mfaransa huyo alijiunga na Simba mapema mwezi Januari akichukua mikoba ya Sven Vandenbroeck ambaye alitimkia Morocco kwenye Klabu ya Far Rabat baada ya kusitisha mkataba wake na Simba.

 

Gomes ameiongoza Simba kwenye mechi tisa hadi sasa ambapo hajapoteza mchezo wowote, mechi mbili kwenye michuano ya Simba Super Cup (Simba 4-1 Al Hilal, Simba 0-0 TP Mazembe), Ligi Kuu Bara mechi nne (Dodoma 1-2 Simba, Simba 2-2 Azam, Biashara 0-1 Simba na Simba 3-0 JKT Tanzania).

 

Michuano ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), mechi moja (Simba 3-0 African Lyon), michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mechi mbili (AS Vita 0-1 Simba, Simba 1-0 Al Ahly).

 

Katika dakika 810, Simba imeruhusu mabao manne huku ikifunga jumla ya mabao 17.Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 45 baada ya kushuka dimbani kwenye mechi 19.


Kesho ina kibarua cha kusaka ushindi mbli ya Al Merrikh kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni hatua ya makundi.

SOMA NA HII  KISA KIPIGO KUTOKA KWA WAMOROCCO...MO DEWJI AIBUKA NA 'KAULI HII YA KIBABE' SIMBA...