Home Simba SC MCHAKATO WA DJUMA WA AS VITA KUTUA SIMBA UKO HIVI..!!

MCHAKATO WA DJUMA WA AS VITA KUTUA SIMBA UKO HIVI..!!


UTAMU wa michuano ya kimataifa umebadili mikakati ya Simba na sasa wameibuka na mikakati mipya ya kusajili vifaa mapema kabisa. Walianza na Perfect Chikwende wa FC Platinum ya Zimbabwe waliyoitoa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Unajua sasa wametua wapi? Unamkumbuka yule beki wa AS Vita aliyekuwa anapanda sana kushambulia almanusura awafunge Simba kule DR Congo. Anaitwa Djuma Shabaan. Viongozi wameshtukia kwamba hana timu nje na wameanza fasta taratibu za kumalizana naye ingawa bado kuna mtihani wa nafasi yake ndani ya Simba kama akija kweli kutokana na umahiri wa Shomari Kapombe.

Shabani katika mechi hiyo ambayo Simba walishinda bao 1-0, likifungwa na Chris Mugalu alionyesha kiwango bora katika kushambulia na alikuwa akiwasumbua Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Luis Miquissone ambao wote walikuwa wakimkaba kwa pamoja.

Wakala Nestor Mutuale ambaye ni mmoja wa mawakala wakubwa huko DR Congo ambaye aliwaleta nchini Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda wa Yanga alidai mchezaji huyo yuko kwenye hatua nzuri ya mazungumzo na Simba.

Kocha msaidizi wa AS Vita, Raoul Shungu alisema kuwa Shabani alimfuata wakiwa nchini Misri walipokwenda kucheza mechi na Al Ahly na kumueleza kwamba Simba wanataka kumpa dili hivyo amshauri.

“Nilimwambia AS Vita hatutamzuia kama Simba watakuja na kufuata taratibu zote sahihi za kiusajili, bado ana mkataba lakini kama Simba watakuja kweli kama ambavyo wamemfuata mchezaji ambaye tayari ametueleza, tutawapatia bila shida,” alisema Shungu.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema Shabani ni mchezaji mzuri ambaye ameonyesha ubora katika mechi yao haswa wakati wa kushambulia lakini alikuwa anamfahamu kabla ya mchezo huo.

“Shomari Kapombe ni mzoefu katika kila mashindano ya ndani na nje ambayo sitamani mchezaji mwingine mbadala wake kwani kiwango chake ni bora sio Simba tu bali Afrika nzima,” alisema.

“Kiukweli nampenda sana Kapombe, anajitambua katika maeneo yote na natamani kuendelea kuwa naye katika timu kwa muda mrefu kwani ni mchezaji mwenye kuelewa anachofanya pamoja na mahitaji ya timu,” alisema Gomes.

SOMA NA HII  GOMES: WACHEZAJI WALIKOSA NAFASI NYINGI ZA WAZI MBALI NA PENALTI

Katika nafasi ya beki wa kulia Simba yupo Kapombe pamoja na David Kameta ‘Duchu’ ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea katika kikosi cha Lipuli na amekuwa hana nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Kikosi cha Simba kina wachezaji kumi wa kigeni na kama watamsajili Shabani maana yake watalazimika kumtoa mmoja kati ya hao lakini pia kuna wachezaji wengine watatu wa kigeni ambao wanatumika katika mashindano ya kimataifa tu.

Wachezaji kumi wa kigeni ni Joash Onyango, Pascal Wawa, Taddeo Lwanga, Larry Bwalya, Clatous Chama, Parfect Chikwende, Meddie Kagere, Chriss Mugalu, Luis Miquissone na Benard Morrison. Watatu wa kigeni ambao wao wanacheza Ligi ya mabingwa Afrika tu ambao ni, Peter Muduhwa, Francis Kahata na Junior Lokosa.