Home Burudani MWAKINYO KUZICHAPA NA MZIMBABWE, KCB YAMWAGA MKWANJA

MWAKINYO KUZICHAPA NA MZIMBABWE, KCB YAMWAGA MKWANJA


  WAKATI bondia Hassan Mwakinyo atapanda ulingoni Machi 26 kuwania  ubingwa wa Afrika (ABU) wa uzito wa Superwelter dhidi ya bondia Mzimbabwe, Brendon Denes, benki ya KCB imetangaza kudhamini pambano hilo kwa Sh 94.4 millioni.

Pambano hilo la raundi 12 limepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Next Door Arena kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa.

Twissa mesema  mkanda huo kwa sasa upo wazi na wameamua Mwakinyo kuwania ubingwa huo ili kumwezesha bondia huyo kuingia katika orodha ya viwango vya shirikisho maarufu la ngumi za kulipwa duniani (WBC).

Twissa amesema kuwa Denes mpaka sasa hajapoteza pambano lolote kati ya nane aliyocheza wakati Mwakinyo amecheza mapambano 18 na kupoteza mawili tu.

Amesema kuwa siku hiyo kutakuwa na mapambano mengine makali  ambapo bondia Jongo Jongo naye atawania ubingwa wa ABU dhidi ya Olanrewaju Durodora wa Nigeria. Pia bondia Ibrahim Class atapanda ulingoni kumsindikiza Mwakinyo kupambana na bondia ambaye atatangazwa baadaye.

“Hii ni sehemu ya pili ya Rumble In Dar na tunaitarajia kuwa kali na kusisimua kwani mabondia wanaopigana ni moto wa kuotea mbali,” amesema Twissa.

Kwa upande wake,  Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa benki ya KCB Christine Manyenye amesema kuwa wameamua kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya pambano hilo ili kuendeleza mchango wao katika maendeleo ya michezo nchini.

Manyenye amesema kuwa benki yao pia inadhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara, mashindano ya Ndondo Cup na riadha ambapo ilidhamini mashindano ya Rock City marathon.

“Ni faraja kubwa kwetu kujihusisha na maendeleo ya michezo nchini  ikiwa pamoja na jamii, hivyo tunatarajia mashabiki wa ngumi za kulipwa watajitokeza kwa wingi siku hiyo na mabondia wa Tanzania watashinda,” amesema Manyenye.

Mkuu wa Masoko wa kampuni ya Multichoice Tanzania, Ronald Baraka Shelukindo amesema kuwa pambano hilo linatarajia kuonekana katika zaidi  ya nchi 30 za bara la Afrika.

Shelukindo amesema kuwa pambano hilo litaonekana kwenye chaneli ya Clouds Plus ambayo ipo kwenye king’amuzi cha DStv na kuwaomba mashabiki wa ngumi za kulipwa kujiunga nacho. Mbali ya benki ya KCB, DStv, pia pambano hilo limedhaminiwa na Onomo Hotel na M-Bet.

SOMA NA HII  TECNO KUWAPA FURAHA WATANZANIA MSIMU WA SIKUKUU NA KOMBE LA DUNIA...

Kwa upande wake, Mwakinyo amesema kuwa amejiandaa vyema na pambano hilo na anatarajia kufanya vyema.

“Nipo kwenye maandalizi kwa ajili ya pambano hilo na ninatarajia kuendeleza wimbi la ushindi.  Muda uliobakia ni mchache sana ambao nautumia kurekebisha na kuboresha mbinu,” amesema Mwakinyo.