Home news PUMZIKA KWA AMANI, KILA KONA MAGUFULI

PUMZIKA KWA AMANI, KILA KONA MAGUFULI


 KILA kona Tanzania kilio! Hiyo ndiyo kauli ambayo unaweza kuisema kufuatia kada mbalimbali za Watanzania ikiwemo ya wanamichezo kuonyesha majonzi mazito baada ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Joseph Magufuli.

Wanamichezo mbalimbali wakiongozwa na klabu kongwe za Simba na Yanga zilionyesha masikitiko yao juu ya kifo cha Rais Magufuli ambacho kilitokea usiku wa kuamkia leo Alhamisi.

 

Taarifa ya msiba wa Rais Magufuli ilitolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) na kueleza kuwa Rais Magufuli amefariki dunia kwa maradhi ya moyo.


Wanamichezo na wasanii mbalimbali kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii hasa ule wa Instagram walionyesha kuguswa na kifo cha Rais Magufuli ambapo waliandika jumbe mbalimbali za majonzi.Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta yeye aliandika: Pigo kwa taifa, pigo kwa Tanzania.

 

Tutakukumbuka daima kwa yote mazuri uliyoyapigania na kuyatekeleza katika vipindi vyako vya uwaziri na urais wa nchi yetu.

 

Haikuwa Dunia ila Mapito. Bwana katoa na bwana katwaa jina lake lihimidiwe.nasi Watanzania. Umeumaliza mwendo mzee wetu, tunakuombea upumzike kwa amani. R.I.P Mr president”Ofisa Mhamashishaji wa Yanga, Antonio Nugaz aliandika: “Haikuwa Dunia ila Mapito. Bwana katoa na bwana katwaa jina lake lihimidiwe.

 

Muigizaji Wema Sepetu aliandika: “RIP MR PRESIDENT…”Nahodha wa Simba, John Bocco aliandika: “Kweli kizuri hakidumu, RIP mzalendo wakweli, Mtanzania uliyeiweka Tanzania mbele na sio ubinafsi naamini wa kujifunza tumejifunza mengi sana kutoka kwako na wakuona tumeona mengi sana mazuri kutoka kwako R.I.P Mr President,


Wewe ni zaidi ya somo kwa Watanzania”Kipa wa Simba, Aishi Manula aliandika: “Daaaaah hakika kwake tutarejea. Binafsi umetekeleza kile Mungu alitaka ufanye kwa Watanzania na huna deni kwetu.

 

Ulale mahali pema peponi”Kiungo wa Yanga, Deus Kaseke: “Rest in peace Mr President, Watanzania tutakukumbuka kwa wema wako uliotutendea hapa duniani”.


Kiungo wa Yanga, Mnyarwanda Haruna Niyonzima aliandika:“Rest in peace President”.


Msemaji wa Simba, Haji Manara aliandika: “PIGO KUU NA MSHTUKO USIOMITHILIKA. Tumshukuru Mungu na kutuliza kama Watanzania”Msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz alisema: “Dah! Jamani”

 

Winga wa Wydad Casablanca, Simon Msuva aliandika: “Pigo kubwa kwa taifa, daima tutakukumbuka kwa yote mazuri uliyotufanyia siwezi kuyasema mangapi katika vipindi vyako vyote vya uwaziri na urais, pole sana Mama Janeth na familia kwa ujumla! Nenda mzee wetu tupo nyuma yako kwa maombi! R.I.P MR.PRESIDENT”.

SOMA NA HII  BAADA YA USHINDI WA MBINDE JANA....GAMONDI KAFUNGA MACHO KISHA AKASEMA HILI...


Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo aliandika:“Ninaishiwa maneno ya kukuelezea mzee wetu, ulikuwa kiongozi shupavu anayependa kuacha alama katika kila jambo unalofanya, mwenye misimamo thabiti kwa manufaa ya taifa letu.

 

“Umejitoa na kufanya mengi makubwa kwa taifa letu, kila mmoja wetu ni shahidi. Vita umevipiga na mwendo umeumaliza baba, pumzika jemedari, pumzika kiongozi wetu, pumzika mzee wetu. Watanzania tutakukumbuka daima.”


Klabu ya Simba SC iliandika: “Pumzika kwa amani Rais wetu mpendwa Dk John Pombe Magufuli. Daima tutakukumbuka.”


Nao Yanga SC waliandika: “Pumzika kwa amani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli Tutakukumbuka milele daima.”


Kuonyesha kwamba yeye ni mwanamichezo haswa enzi za uhai wake Dk Magufuli aliwahi kusema:

 

“Mimi huwa nafuatilia timu, na huwa nafuatilia ligi mbalimbali za hapa nyumbani na hata za nje. Katika kufuatilia timu mbalimbali hadi Jumamosi iliyopita niligundua kuwa zimebaki timu mbili tu ambazo zimechukua ubingwa bila kufungwa, zilikuwa Simba na Barcelona ya Hispania.

 

“Lakini Jumamosi usiku Barcelona ikawa imefungwa hivyo nikawa nafikiri imebaki tu Simba lakini leo na yenyewe Simba imefungwa. Hata hivyo nikaona sina budi kukubali mwaliko huu wa kuwapongeza Simba kwa kufungwa bao moja tu leo.


“Hasa kwa kuzingatia kuwa imepitia kipindi kirefu bila kuchukua ubingwa.Nawapongeza sana wachezaji, viongozi na msemaji wenu, Manara ingawa leo namuona hana raha kwa kuchukua ubingwa kwa staili hii japo siyo mara ya kwanza.


“Nazipongeza timu nyingine zilizoshiriki kwa kuonyesha ushindani mkubwa na kukubali matokeo.

 Nimefurahi msimu huu hakuna timu iliyokwenda Fifa kudai pointi za mezani, timu zote zimekubali matokeo.


“Kwa namna ya pekee ninawapongeza Kagera Sugar wamecheza mchezo mzuri mbele ya umati wa washangiliaji hawa lakini wametoboa tundu la Wanasimba.

 

“Ni lazima tujifunze kushangilia hata wale wanaotuzidi katika michezo, hii pia inatusaidia kutupa changamoto sisi Wanasimba na kwa wachezaji wengine wa Tanzania.

 

“Ninaposema Wanasimba sio mimi mimi natoa changamoto, hii inatoa changamoto kubwa kwa timu zetu za taifa zinapofanikiwa kushinda ziwe zinaweka mazingira ya kujiamini na kujipanga kisawasawa katika kushinda michezo mikubwa zaidi.


“Kwa sababu kwa timu kama Simba ambayo haikuwa imefungwa katika kipindi chote kushindwa leo ni dosari kubwa. Na hii mimi nawaeleza ukweli na ukweli utabaki kuwa ukweli lakini nawapongeza kwamba ushindi huu ututasaidia kulileta kombe la Afrika hapa nchini,” alisema Dk Magufuli enzi za uhai wake.