Home Simba SC SIMBA SC WAPEWA MBINU ZA KUEPUKA KUFUNGWA MAGOLI YA ‘FAULO’

SIMBA SC WAPEWA MBINU ZA KUEPUKA KUFUNGWA MAGOLI YA ‘FAULO’


KOCHA Didier Gomes, juzi nusura atibuliwe rekodi zake Simba kama sio bao la jioni la Luis Miquissone kumpa sare ya kwanza katika Ligi Kuu, lakini sasa akapewa mbinu ambazo akizitumia zitamuepushia presha kutoka kwa mabeki wakisaka heshima ndani na nje ya nchi hasa mipira ya faulo.

Simba ililazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwa kuchomoa bao jioni, huku wakikosa penalti iliyopatikana kipindi cha kwanza na kuruhusu bao la friikii lililokaribia kuwatia aibu kwa mara ya pili mbele ya maafande hao waliowafunga pia mechi ya kwanza.

Gomes na wenzake wamepewa mbinu za kufanya ili kuiepusha timu dhidi ya mabao ya friikikii ambayo imeonekana ni tatizo kwa timu kwa misimu mitatu mfululizo sasa, likiwamo la juzi lililofungwa na Salum Kimenya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar.

Straika wa zamani wa Azam FC, Phillip Alando alisema Simba inatakiwa ifanye mambo mawili kumaliza tatizo hilo vinginevyo linaweza kuwagharimu mara kwa mara hasa katika mashindano ya kimataifa ambayo wanashiriki.

“Nahisi kinachowaangusha Simba ni kukosa mchezaji kiongozi ambaye atakuwa anaipa mwongozo timu pindi inapopigiwa mipira ya faulo au kona, hivyo wanajikuta wanashindwa kujipanga vyema na kukosa mtu wa kuwakumbusha majukumu pale wanapopanga ukuta. Nakumbuka Azam ile iliyochukua ubingwa wa Ligi Kuu, kazi hii ilikuwa inafanywa na Said Morad,” alisema Alando.

“Na mtu wa aina hii anatengenezwa, hapatikani kirahisi tu. Lakini kingine wanachotakiwa kufanya ni kuanza kuepuka kufanya makosa jirani na eneo la hatari kama wanaona ni vigumu kwao kuokoa mipira ya adhabu ndogo. Kama ni faulo basi zifanyike mbali na eneo la hatari vinginevyo wataendelea kuruhusu mabao ya namna hiyo.” 

Naye nyota wa zamani wa Simba anayeinoa Pamba FC, Ulimboka Mwakingwe alisema kitendo cha Simba kuruhusu mabao ya faulo ni tatizo linalotakiwa kutafutiwa tiba haraka. “Inawezekana benchi la ufundi limekuwa halifanyii sana kazi mazoezini suala la kuzuia mipira ya adhabu ndogo, lakini siku zote makosa yanapotokea ndio yanakupa nafasi kocha kufanyia kazi mazoezini, hivyo sina shaka kocha wa Simba na benchi la ufundi watashughulikia tatizo hili,” alisema Ulimboka.

SOMA NA HII  HIZI HAPA DAKIKA ZA KUFA KUPONA KWA SIMBA NA YANGA CAF....WAKISHINDWA NDIO BASI TENA...

“Simba ina mechi za kimataifa dhidi ya timu nzuri, hivyo kufungwa mabao ya aina hiyo kwa kujirudia dhidi ya timu kama Prisons ni lazima benchi la ufundi kufanyia kazi na sina shaka na hilo kwa sababu makosa kwenye soka yapo na siku zote makocha tumekuwa tukijifunza na kufanyia kazi.”

Hata hivyo, Kocha Gomes alisema hawezi kumlaumu mchezaji yeyote kutokana na bao hilo licha ya mazoezi ya mara kwa mara ya kukabiliana na mipira ya faulo. “Siku zote nimekuwa nikisema kuwa siwezi kumlaumu wachezaji wangu. Tunafanyia kazi sana mipira ya kutenga, kona na penati.Kwenye ulinzi tuko imara kwa sasa,” alisema Gomes.

Kilichofanywa na Kimenya ni sawa na kilichofanywa na mshambuliaji Bernard Morrison ambaye aliwafunga Simba bao la mkwaju wa faulo wakati huo akiichezea Yanga msimu uliopita katika mchezo ambao timu yake iliibuka na ushindi wa bao 1-0 mzunguko wa pili Ligi Kuu.

Kabla ya hapo, winga Luis Miquissone ambaye kwa sasa anaitumikia Simba, aliwanyima nafasi ya kutinga raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita baada ya kuwafunga bao kwa mkwaju wa faulo akitumia makosa ya ukuta katika mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 wakati huo akiwa anachezea UD Songo ya Msumbiji.

Lakini pia msimu huohuo, Simba iliruhusu pia bao la faulo la beki Israel Patrick katika mchezo wake dhidi ya Alliance ya Mwanza.