KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes, amewataka wachezaji wake wote wa kigeni waliopo kwenye majukumu ya timu za taifa kuhakikisha wanaripoti kambini Machi 30, mwaka huu ili kuendelea na maandalizi ya mechi za kimataifa.
Miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao wapo kwenye timu zao za taifa ni pamoja na Perfect Chikwende, Luis Miquissone, Clatous Chama, Meddie Kagere, Shomari Kapombe, Mohamed Hussin, Aishi Manula.
Simba itavaana na AS Vita, Aprili 3, mwaka huu mchezo utakaopigwa saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Kocha amesitisha mazoezi kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu lengo ni kuhakikisha wanasubiri wachezaji waliopo kwenye timu za taifa ili watakapojiunga waanze program ya pamoja kwani awali walikuwa wakifanya nane tu mazoezi.
Timu hizo zitavaana katika mchezo wa tano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ule wa awali uliopigwa huko Kinshasa, Congo ulimalizika kwa Simba kushinda bao 1-0 ambalo lilifungwa na Mkongomani Chris Mugalu.
Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu alisema kuwa tayari wamewapa taarifa wachezaji wao wote waliopo timu za taifa kuhakikisha wanaripoti Machi 30 wakati timu zote zitakapomaliza michezo ya timu za taifa.
“Tumepanga wachezaji waliopo katika timu za taifa kuripoti kambini hadi kufikia Machi 30 kwa wale wa kigeni.
“Wachezaji wa kigeni wengi mechi zao zinachezwa kati ya Machi 29 na 30, mwaka huu hivyo mara baada ya michezo hiyo haraka watatakiwa kuungana na wachezaji wenzao waliopo Stars kwa ajili ya kuanza maandalizi ya AS Vita,” alisema Rweyemamu.
Chanzo: Championi