Home Ligi Kuu TIMU ZA BONGO ZIMEACHIWA DENI LA KULIPA NA MAGUFULI

TIMU ZA BONGO ZIMEACHIWA DENI LA KULIPA NA MAGUFULI


LICHA ya kwamba Simba wanacheza soka la pasi nyingi ambalo wengi wanapenda kuliita pira biriani ila bado wana deni kwa Rais John Pombe Magufuli la kuleta kombe la Afrika kwenye ardhi  ya Tanzania.

Magufuli ametangulia mbele za haki akiwa ameacha alama ya kusimamia ukweli pamoja na kuona yale ambayo anahitaji yakitokea ila bado ameacha deni kwa timu zote za Tanzania.

Agizo lake la kuona kwamba Simba ama timu nyingine inaleta Kombe la Afrika kwenye ardhi ya Tanzania haitafutika kwa kuwa maneno yanaishi.

Ukiweka kando agizo la kuitaka Simba na timu nyingine ambazo ni Yanga, Azam FC, Kagera Sugar, Azam FC kuleta kombe la Afrika bado alikuwa anasisitiza kuhusu umoja.

Ile Kasumba kwa timu kutengana hasa kwenye mashindano ya kimataifa alikuwa anachukia na hakuwahi kupenda suala hilo kabisa zama za uhai wake.

Aliweka wazi kwamba inahitajika umoja na mshikamano katika mashindano ya kimataifa kwa timu zote na mashabiki wote.

Magufuli alisema kuwa ikitokea Yanga itakuwa inacheza mashindano ya kimataifa ama ikitokea Simba itakuwa inacheza mashindano ya kimataifa basi ni lazima mashabiki waungane washangile timu ambayo itakuwa uwanjani.

Bado kwenye mpira ameacha alama na neno lake kwa wizara ya michezo alikuwa anahitaji kuona timu ya Taifa ya Tanzania inapata matokeo chanya kila wakati.

Ni aina ya maisha ambayo yalikuwa kwenye kasi kubwa lakini kila kitu kilikuwa kinaonekana na leo inabaki kuwa historia.

Msema ukweli, mchapakazi, mpenda michezo na burudani leo amemaliza mwendo ila ameacha maagizo ambayo yanapaswa yatimizwe kwa vitendo na kila mmoja.

Ikiwa utahitaji kuandika ama kusema yale ambayo ameyafanya Magufuli itakuwa ngumu kuyamaliza yote kwani kila sekta alikuwa anafanya na kuacha alama.

Mpenda michezo, mpenda maendeleo mpenda kazi na mzalendo wa kweli katika awamu ya tano ni alama ambayo inaishi muda wote.

Katika kipindi hiki ni muhimu kwa kila timu kujipanga na kutimiza majukumu ambayo yanawahusu ili kuweza kufikia mafanikio ambayo ni ndoto ya kila mmoja.

SOMA NA HII  VPL: POLISI TANZANIA 0-1 SIMBA, CCM KIRUMBA

Matabaka ambayo yamekuwa yakijengwa kila siku yanaturudisha nyuma na kutufanya tubaki pale ambapo Magufuli pamoja na viongozi wengi wapenda maendeleo walikuwa wanayakataa.

Kwa sasa ni muda wa kufanya kwa vitendo na kuendelea kupambana ili kuweza kuona kila kitu kinatokea. Kwa kufanya hivyo itakuwa ni njia sahihi ya kumuenzi Magufuli kwa vitendo.

Muda ambao umebaki kwa sasa ni kuendelea kutimiza kazi zetu kwa vitendo. Hakuna ambaye anapenda kufeli hivyo ili kufaulu ni lazima kufanya kazi kwa juhudi na kuwa na mipango makini.

Tumekuwa tukiona kwamba wapo ambao wanajitokeza kuwapa sapoti wapinzani wa timu moja inapocheza kimataifa, tuliona wakati ule kulikuwa na mashabiki ambao ni Watanzania walikuwa wanakwenda kuwapokea wapinzani wa Simba.

Ni zama za kuungana na kuenzi yale ambayo Magufuli alikuwa anahitaji kuona yakitokea. Wakati wa kuwa wamoja ni sasa na zile tofauti zote ziwekwe kando.