KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, viongozi wa Klabu ya AS Vita juzi Alhamisi walikataa basi ambalo waliandaliwa na wenyeji wao Klabu ya Simba mara baada ya kuwasili nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nyerere.
AS Vita walifika nchini Alhamisi saa moja usiku ambapo baada ya kumalizika kwa shughuli za ndani, kwa maana ya kukaguliwa walitakiwa kupanda basi ili waweze kwenda hotelini kwa ajili ya kupumzika.
Lakini mambo yalikuwa tofauti mara baada ya viongozi wa timu kukataa kupanda basi aina ya Yutong la Kampuni ya Happy Nation ambalo liliandaliwa na klabu wenyeji wao ambao ni Simba kama sheria inavyohitaji timu mwenyeji kuwaandalia usafiri timu ngeni.
Katika hali ya kushangaza, gari la kisasa la Klabu ya Azam FC ndilo lilitumika kuwabeba wachezaji na viongozi wa Klabu ya AS Vita na kuwapeleka hotelini.
Mchongo mzima wa kulikataa basi hilo uliandaliwa mapema na Meneja wa AS Vita, Yves Diba Ilunga ambaye alifika nchini tangu Jumanne iliyopita kwa ajili ya kuweka mambo sawa.
Hata Hivyo Championi Jumamosi, lilimuuliza Meneja wa AS Vita juu ya kulikataa basi hilo lakini hakuweka wazi na kusisitiza kuwa tayari walishakuwa na usafiri wao na hakukuwa na sababu ya kutimia usafiri mwingine.