MOJA kati ya jambo ambalo linawatesa wachezaji wengi waliocheza soka miaka ya nyuma ni kuwa, nyakati zao hawakuwa vizuri katika suala la malipo, na hata wale wachache waliopata bahati ya kulipwa vizuri wengi wao hawakutumia fedha hizo katika mazingira mazuri kwao.
Naelewa kuwa miaka kuanzia 10 kurudi nyuma kuna wimbi kubwa la wachezaji ambao walikuwa na vipaji vya juu, majina makubwa na waliwika hasa uwanjani lakini bahati mbaya kwenye malipo hakukuwa na mifumo mizuri ya kuwawezesha wao kuneemeka kama ilivyo kizazi cha sasa.
Wachezaji wa wakati huo walitegemea washinde mechi hasa zile dhidi ya wapinzani wa jadi au timu kubwa ndiyo wapewe posho zilizonona, baadhi yao wakatumia majina yao kupata senti kadhaa mitaani na kwenye kumbi za starehe.Wapo wachache ambao walikumbuka kujipanga na kujua kuwa kuna maisha baada ya soka.
Kwa kawaida mchezo wa soka licha ya kuwa na faida kubwa na kupendwa na watu wengi duniani kuliko michezo mingine yote, lakini kwa wachezaji huwa wana muda mfupi wa kucheza katika ubora wa juu kuliko ajira nyingine.
Kwa kawaida ni nadra kukuta mchezaji akicheza katika ubora wa juu kwa miaka 10 mfululizo, wengi wanacheza miaka mitano kwa kiwango bora baada ya hapo wanakuwa wachezaji wa kawaida na matokeo yake thamani yao inashuka.
Simba na Yanga ndizo klabu ambazo zimekuwa na kawaida ya kusajili wachezaji kwa thamani kubwa na kuwalipa mishahara mizuri, mbali na hapo kuna dau la usajili na posho nyingine za hapa na pale.
Azam FC nayo ikaibuka miaka ya hapo kati na kuingia katika orodha ya timu ambazo zimekuwa zikifanya vizuri pia kwenye suala la uchumi, hilo ni jambo zuri na binafsi huwa natamani zitokee timu kama Azam FC zaidi ya tatu au nne kwenye soka la Tanzania, ikiwa hivyo hata ushindani utabadilika na kuwa mkali zaidi ya ilivyo sasa.
Ukitamaza msimamo wa Ligi Kuu Bara utaziona timu hizo ndizo ambazo zipo kwenye nafasi tatu za juu, hiyo inathibitisha hiki ninachokisema kuwa soka ni fedha, ukiwa vizuri kiuchumi unaweza kufanya mambo makubwa.
Hivyo wakati Tanzania inazungumzia klabu kufanya vizuri kwa kuwa zipo vizuri kiuchumi, huu ni muda wa wachezaji nao kutafakari kuwa kuna maisha baada ya soka au kuna maisha baada ya kumaliza kucheza soka, na hayo ni marefu zaidi kuliko hiyo ajira yao ya sasa.Kucheza soka kunaendana na umri, kuna hatua ikifika hata kama bado akili yao inajua hapa natakiwa nifanye hivi au vile lakini umri unauzuia mwili, mwisho wake hauwezi kufanya kile unachowaza kichwani.
Hivi karibuni kulikuwa na tetesi juu ya beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein maarufu kwa jina la Zimbwe Jr au Tshabalala kuwa anawaniwa na Yanga, ikielezwa kuwa kuna uwezekano mkubwa msimu ujao akatua kwa timu hiyo ya Jangwani.
Hii kwangu mimi naiona ni moja kati ya habari nzuri kwa faida ya soka la Tanzania, kwa faida ya wachezaji wazawa na kwa faida ya Zimbwe Jr mwenyewe.
Kama ni kweli Yanga wanataka kumsajili inamaanisha kuwa itakuwa ni nafasi nzuri kwa pande hizo nilizozitaja juu kuneemeka kwa njia tofauti.Kwa soka la nchi itaongeza ushindani, kwa wachezaji wazawa itaongeza thamani yao na kwa Zimbwe Jr mwenyewe itaongeza thamani yake na anaweza kupata fedha ambazo inawezekana hatazipata tena katika maisha yake ya kucheza soka.
Hivyo, huu ni wakati wa Zimbwe Jr kufanya maamuzi sahihi akitambua kuwa miaka michache ijayo umri wake wa kucheza soka utafikia ukomo na atakuwa na maisha mengi nje ya uwanja, binafsi namshauri popote ambapo kutakuwa na faida kimaslahi na faida ya uwanjani basi aelekee huko.