Home Taifa Stars BILA KUJIPANGA KOMBE LA DUNIA MAMBO YATAKUWA MAGUMU PIA KWA STARS

BILA KUJIPANGA KOMBE LA DUNIA MAMBO YATAKUWA MAGUMU PIA KWA STARS

KWA sasa suala la timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kushiriki Afcon imebaki kuwa ndoto tu kwani kikosi hicho kilikosa nafasi hiyo baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi lake J ambalo walipangwa.
Kushindwa kwa Stars kulitokana na sababu nyingi lakini kupoteza mechi zote za ugenini kwenye kundi lake ilikuwa moja ya sababu ambazo ziliwanyima nafasi hiyo. Kwa muda huu suala hilo linatakiwa liwekwe kando kwa sababu hata tukilizungumza kwa namna gani haliwezi kubadilika.
Kitu kilichopo mbele kwa sasa kwa timu hiyo ni kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022 ambalo litafanyika kule Qatar. Tayari Stars washajua aina gani ya maadui ambao wataenda kukutana nao kwa sababu wameshapangiwa kundi.
Kikosi hicho kinachofundishwa na kocha Kim Poulsen raia wa Denmark kimepangwa kwenye kundi J kikiwa sambamba na timu za nchi za DR Congo, Benin na Madagascar.
Kwa kujua huku mapema aina ya wapinzani ambao wamepangwa nao kwenye hatua hiyo ni vyema wakaanza maandalizi mapema kwa ajili ya kuweka matumaini ya kufuzu kwa hatua inayokuja.
Kama hakutakuwa na maandalizi mazuri kwa ajili ya michuano hii nadhani hata huku tutakosa nafasi ya kucheza michuano kama ambavyo imekuwa kwenye Afcon.
Wasimamizi wote wa timu hiyo nadhani sasa ndiyo muda wa kuanza kuweka mikakati mizuri juu ya michuano hiyo kwa sababu ndiyo ambayo itapoza mioyo ya Watanzania baada ya kukosa nafasi ya kwenda Afcon.
Kama inawezekana ni vyema kuanza kuzichunguza timu pinzani kwa wakati huu kujua namna zinavyocheza, kutazama ubora na makosa yao ili tutakapokuja kupambana nao iwe rahisi kupata ushindi.
Uzuri ni kuwa kila kitu kinapatikana mtandaoni na hivi karibuni tuliwahi kucheza na DR Congo hivyo inaweza kutumika kama moja ya silaha ya kuwatazama wapinzani kwa lengo moja tu la kupata matokeo kwa kipindi ambacho watakapocheza.
Hii ndiyo nafasi pekee ambayo wachezaji na benchi la ufundi la Stars linaweza kuitumia kwa ajili ya kuwapoza mashabiki zao ikiwa ni baada ya kushindwa kwenda Afcon lakini kusipokuwa na mikakati mizuri basi hata kufuzu Kombe la Dunia napo kunaweza kuwa historia tu.
Lakini nataka kuwakumbusha pia Simba juu yaoya mwisho dhidi ya Al Ahly kuwa wana kazi ngumu ya kuweza kujipima kuona namna gani wanaweza kupata matokeo ugenini mbele ya wababe wenye hasira ya kufungwa walipokuja Bongo.
Pamoja na kwamba mmefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali bado mna kazi ya kufanya kwenye mechi hiyo ya kumaliza katika hatua ya makundi.
Ile rekodi yenu ya kutokufungwa inawezekana na ipo wazi ikiwa mtadhamiria kufanya hivyo ugenini hapo Aprili 9.
Kushinda ama sare kwenu itakuwa kipimo cha kuweza kufikia malengo ya hatua ya nusu fainali ambayo mmejiwekea kwa sasa ili muweze kuyafikia.
Hivyo wachezaji pamoja na benchi la ufundi la Simba linatakiwa kukumbushana kupambana kupata ushindi katika mechi hii ambayo ni muhimu kwenu katika kupata picha ya kile ambacho mnakipigia hesabu.

SOMA NA HII  KOCHA WA TIMU YA TAIFA POULSEN ATAKA WACHEZAJI KUJITUMA