Home Uncategorized KARIA – KLABU ZA LIGI KUU ZIJITAMBUE

KARIA – KLABU ZA LIGI KUU ZIJITAMBUE

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amezitaka klabu zinazoshiriki Ligi nchini kujitambua zikiwemo Simba na Yanga.

Bosi huyo wa soka nchini amekwenda mbali zaidi na kueleza kwamba kama klabu zitajitambua, ufanisi zaidi utaongezeka kwenye Ligi wanazoshiriki.

Karia ambaye ni mgeni rasmi kwenye mkutano mkuu wa saba wa Bodi ya Ligi amesema Ligi sasa ni ya Bodi na klabu shiriki, hivyo wanapaswa kuisimamia ili iwe bora zaidi.

“Kila msimu tunatamani Ligi iwe bora, lakini itakuaje bora? ni wasimamizi na klabu shiriki kujitambua na kuifanya kwa ufanisi zaidi,” amesema Karia

Amesema hivi sasa Ligi inasimamiwa kwa asilimia 100 na Bodi na haiko TFF.

“Japo utaratibu wa kisheria ili ijitegemee bado haujakamilika, lakini Bodi tayari imeanza kujitegemea na Ligi wanaisimamia wenyewe,” amesema Karia

Amesema mchakato wa Bodi kujisajili bado, ingawa wataamua wenyewe wajisajili kama kampuni au vinginevyo.

Ingawa nje ya mkutano, mwanasheria wa TFF alisema kuna ugumu Bodi kujitegemea moja kwa moja kwa mujibu wa sheria.

“Bodi ya Ligi ni chombo ambacho kimeundwa chini ya TFF, hadi kianze kujitegemea ni process (mchakato), ni kama mahakama ya wilaya na mahakama kuu, kutengana ni ngumu,” amesema.

Kingine ambacho Karia amekisisitiza kwenye mkutano huo ni klabu kuwa na programu za vijana.

“Wale inaowapandisha pia ziwape nafasi ya kucheza ili kuimarisha viwango vyao, lakini pia kutasaidia kuwa na timu imara ya taifa ya vijana,” ameeleza Karia na kuongeza;

“Klabu pia ziishi kwenye mfumo wa club licensing, hili ni jukumu la Bodi kulisimamia, tukifanikiwa kwenye hili tutapiga hatua zaidi,”

Wakati huo huo, Karia ameagiza uwanja wa Majimaji wa Songea kutotumika kwenye mechi zozote za Ligi hadi utakapofanyiwa marekebisho.


Credit – Mwanaspoti

SOMA NA HII  NYOTA ANAYEMKIMBIZA KAGERE MDOGOMDOGO ATAJA KINACHOMBEBA