Home Yanga SC KUMEKUCHA YANGA, KOCHA HUYU KUPEWA MIKOBA YA KAZE

KUMEKUCHA YANGA, KOCHA HUYU KUPEWA MIKOBA YA KAZE


 UONGOZI wa Yanga, unatarajiwa 
kumpokea kocha ambaye ataifundisha timu hiyo akichukua mikoba ya Mrundi, Cedric Kaze aliyetimuliwa Machi 7, mwaka huu.

Makocha wawili mpaka sasa ndiyo wanatajwa kwamba mmoja wao anaweza kuinoa Yanga ambapo makocha hao wote wamepita Al Merrikh ya Sudan ambao ni Mserbia, Miodrag Ješić na Mtunisia, Nasreddine Nabi.

Ješić ndiye alikuwa wa kwanza kutua Al Merrikh ikiwa ni siku chache tu tangu Didier Gomes kuachana na timu hiyo na kutua Simba alipo sasa.

Siku mbili baada ya Al Merrikh kumtambulisha Ješić kama Mkurugenzi wa Ufundi, ndipo Nasreddine akatambuliwa kuwa kocha mkuu, akaiongoza timu hiyo kwenye mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika akipoteza dhidi ya Al Ahly na AS Vita, kisha sare na Simba, akatimuliwa.

Timu ikakabidhiwa kwa Muingereza, Lee Clark ambaye anainoa timu hiyo kwa sasa ikiwa imeishia hatua ya makundi.

Wakati Yanga ikiwa kwenye mchakato wa kumpata mrithi wa Kaze, makocha wengi wamehusishwa akiwemo Nikola Kovazovic, Hubert Velud, Sebastian Migne, kabla ya kuibuka kwa makocha hao wawili.

Chanzo chetu kimeliambia Spoti Xtra kuwa, tayari Kamati ya Utendaji ya Yanga, imeshampata kocha ambaye atakuja kuinoa timu hiyo ambayo kwa sasa ipo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi.

“Baada ya kupitia CV nyingi na kujiridhisha juu ya kocha tunayemuhitaji, Jumapili au Jumatatu, tutakuwa na kazi ya kumpokea kocha wetu mwenye CV kubwa sana Afrika, maana ni kocha aliyewahi kuzinoa moja ya timu kubwa za Sudan.

“Tayari tumeshafanya maandalizi yake kwa maana ya kumtumia tiketi na mapokezi, japo ratiba ya ndege ya nchi anayotokea ambayo siwezi kukuambia kwa sasa ilikuwa na mkanganyiko, lakini mambo yamekaa sawa na ndani ya siku mbili hizi nilizokwambia atakuja kujiunga nasi,” kilisema Chanzo hicho.


SOMA NA HII  MAJANGA MKUDE AMFUNGULIA MASHTAKA MO DEWJI ADAI FIDIA KISA HIKI HAPA