BEKI wa kati wa Klabu ya Yanga, Abdalah Shaibu,’Ninja’ amesema kuwa anawatambua vizuri wapinzani wake Simba hivyo hana mashaka kuelekea kwenye mchezo wao ujao ikiwa atapata nafasi ya kuwazuia wasiwafunge.
Ninja ameanza kuaminika kikosi cha kwanza huku akipewa ujumbe na viongozi wa Yanga kwamba aendelee kupambana kwa ajili ya timu hiyo inayopambana kutwaa taji la Ligi Kuu Bara lililo mikononi mwa Simba.
Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Antonio Nugaz ambaye ni Ofisa Uhamasishaji wa Yanga. Mei 8 Uwanja wa Mkapa anatarajiwa kuwa na kazi ya kuzuia mashambulizi ya Meddie Kagere, Clatous Chama na Luis Miquissone.
Beki huyo mzawa amesema:”Ninatambua kwamba Simba ina wachezaji ambao ni wasumbufu ila bahati nzuri ni kwamba hao nimewahi kukutana nao uwanjani na ninajua mbinu zao.
“Labda mmoja bado ambaye ni Luis, lakini naye pia ninajua namna anavyocheza hivyo ni suala la kuomba uzima ili kila kitu kiwe sawa,” .
Mchezo wa kwanza walipokutana ubao ulisoma Yanga 1-1 Simba hivyo mchezo ujao utakuwa na ushindani kwa kuwa timu zote zinahitaji kutwaa taji la ligi.
Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 27 na Simba ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 61 baada ya kucheza mechi 25.