UONGOZI wa Namungo umeweka wazi kuwa unahitaji kulitwaa taji la Kombe la Shirikisho ili iweze kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo makubwa Afrika kwa mara nyingine tena.
Namungo kwa mara ya kwanza imefanikiwa kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi.
Mchezo wa mwisho uliopigwa Aprili 28, mwaka huu Cairo nchini Misri dhidi ya Pyramids, Namungo ilipoteza kwa bao 1-0 lililofungwa na Ibrahim Adel dakika ya 65.
Haikuwa na bahati katika mechi zote ilizocheza kwa kuwa haikukukusanya pointi wala kufunga bao katika mechi zote za mashindano.
Ofisa Habari wa Namungo, Kindamba Namlia amesema: “Tupo imara na tunajua kwamba hatukuwa kwenye mwendo mzuri, tutapambana tukirudi kwa kuwa uzoefu tumepata.
“Licha ya kupoteza michezo yote lakini tumepata uzoefu mkubwa ambao utatusaidia kwa msimu unaokuja, tunaamini tutafanya vizuri kwenye kombe hili na kusonga mbele hivyo tunahitaji kutwaa ubingwa ” amesema Kindamba.
Jana, Namungo ilipenya hatua ya robo fainali baada ya kushinda mabao 3-2 dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora Kombe la Shirikisho.