MSEMAJI wa Klabu ya Simba SC, Haji Manara, leo Mei 07 amefika katika Studio za +255 Global radio zilizopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam na kufanya mahojiano na Kipindi cha Krosi Dongo kuelekea mchezo wa Dabi ya watani wa jadi kati ya Simba na Yanga, utakaopigwa kesho Mei 8, 2021 katika Dimba la Mkapa.
Alichokisema Manara
“Mimi napata presha ya mchezo ile hali ya kawaida kuelekea mechi ya Watani wa Jadi, baada ya matokeo kuna kucharurana, hii tumeshaizoea ni hali ya kawaida ya mchezo, inatokea mara moja au mara tatu kwa mwaka, siwezi kusema ni presha ni hali ya mchezo.
“Sipati presha ya mchezo wa Simba na Yanga labda mechi zile za Klabu Bingwa, mfano Al Alhy au AS Vita usije ukafungwa ukaabika.
“Kuna kitu kinawekwa ili kufifisha uhalisia, kwa miaka mitano mfululizo (2016-2021) kwenye Ligi Kuu, Yanga amemfunga Simba mara moja tu. Lakini inawekwa kama Simba hapati matokeo, sasa hesabu Simba kamfunga Yanga mara ngapi.
“Mpira wetu umekuwa kama siasa lazima mtu ‘a-balance’, Yanga kutoa sare imekuwa kama credit. Sisi tumewafunga nne, wao wametufunga bao 1 la Morrison. Kwenye takwimu hakuna mechi hata moja Yanga ame-poses dhidi ya Simba, haipo.
“Matokeo ya mpira yanategemea mambo mengi sana, wakati mwingine ni bahati au ujanja ujanja, lakini sioni Yanga kwamba wamepata matokeo mazuri kwa sababu wamepata droo, wao sio Prisons, wao ni timu kubwa, wasijiandae kushangilia droo.
“Haiwezekani timu bora ikafungwa na timu dhaifu, ni vitu viwili viwaweza kusababisha, moja ni bahati, mbili ni ujanja ujanja, sitaki kusema ni ujanja upi.
“Bahati nzuri niko kwenye uongozi wa Simba kwa muda mrefu, siku nikimaliza career yangu naweza kuja kuwa hata Rais wa FIFA, ukiwa kiongozi wa Simba au Yanga kwa muda mrefu, unakuwa unajua mipango ya mpira.
“Ndio maana kama nchi tunafika mahali tuna-stack, kuna wakati Simba na Yanga tulikuwa tunalaumiwa sijui hivi mara vile, lakini tunapokwenda kwenye mashindano ambayo ujanja ujanja hautumiki Simba tunafanya vizuri sana.
“Simba hakuna mchezaji yeyote wa Yanga tunayemhofia, tunawaheshimu wachezaji wote ni wazuri. Simba imekutana na wachezaji wazuri kwenye mashindano mbalimbali msimu huu. tumemfunga Al Ahly, kwake akatufunga bao 1, dakika 30 za mwisho akapaki basi, hatumhofii Yanga.
“Ukubwa wa Yanga hapana, labda ukongwe tu. Wachezaji wa Yanga huwezi kulinganisha na AS Vita, Al Merreikh au Al Ahly. Unamhofu nani, unahofu nini? Hapana. Kwanza sasa hivi baada ya chai, wachezaji wetu wanacheza game (play station).
“Mechi tuliyotoa sare na Al Merreikh kwao hatukupata ugumu wowote, plan ya mwalimu ya away ndio ilitusaidia, ndio maana kocha wao ambaye kwa sasa ndiyo kocha wa Yanga, usiku uleule alifukuzwa kazi.
“Kocha wetu yuko tofauti sana, anawasoma mapema wapinzani wetu kabla ya mechi. Kocha wa Simba anawajua wachezaji wa Yanga kuliko Kocha wa Yanga, anafuatilia mechi nyingi na muda wote anaagalia mpira na mtu wake wa analysis pamoja na Matola.
“Kocha wetu anawapa mbinu wachezaji namna wapinzani wetu wanavyocheza na ni bingwa wa kubadilisha mbinu.
“Gomes alikuwa akiifundisha Al Merreikh, alivunja mkataba wake ili aje kuifundisha Simba, Nabi alikuwa akifundisha Al Merreikh, alifukuzwa na sasa anafundisha Yanga, tofauti ya Kocha aliyefukuzwa na aliyevunja mkataba hawa ni watu wawili tofauti.
“Yanga hawawezi kufunga mbele ya Simba, mbinu watakayokuja nayo ni kupaki basi ili watumie counter attack, mbinu ya pili wanadhani itawasaidia kucheza rafu na kugongana gongana.
“Bernard Morrison ambaye anaweza kuanza au kutokea benchi, huyu akipewa dakika 35, atafanya mchezo wa kesho kuwa mwepesi sana. Morrison sasa hivi sio selfish tena, hachezi na jukwaa anacheza kwa ajili ya timu. Usimfananishe Morrison na Yacouba? Hapana, control yenyewe kapata wapi?
“Mechi ya kesho Simba hatutaki kubebwa wala Yanga kubebwa, tunataka dakika 90 za haki. Ikitokea Simba tumefungwa bao 5 na mchezaji wa Simba akafanya ‘faulo’ ndani ya 18, kama kadi nyekundu apewe na penati itengwe ili Yanga afunge bao la 6.
“Kwenye mechi za Simba na Yanga usipotenda haki hasa masuala ya ‘faulo’ unaharibu mpira. Refa wa kesho tutajua amemudu mpira dakika 10 za mwanzo, akitoa njano tatu dakika za mwanzo mpira utatulia mpaka mwisho. tunataka kuona football sio rafu wala kubebwa.
“Mimi sioni ubora wowote wa Yanga labda ukongwe. kipindi cha nyuma ndio walikuwa wana ile kujituma lakini kwa sasa haipo. Fighting spirit ya Simba ni kubwa kuliko Yanga, spirit sio kukimbia sana ni kutafuta bao na kufunga.
“Ninaapa kwa jina la Quran na huu ni Mwezi Mtukufu, kwa miaka hii saba hakuna siku ambayo viongozi wa Simba wamempangia kikosi mwalimu, kwanza unaanzaje? Haya mambo yanatengenezwa tu mtaani. Hata Yanga wenyewe huwezi. Yule Kocha Sven hata kiongozi ukienda mazoezini anakufukuza, unaanzaje kumpangia kikosi?
“Kihalali kabisa, kama hakuna ujanja ujanja, hakuna mipango, hakuna hujuma, hakuna asante refa, Simba anamfunga Yanga bao 4 kesho kwa Mkapa, hizo ni chache.
“Hata tukifungwa na Yanga kesho, mpango wetu wa ubingwa uko palepale sababu tutakuwa bado tunaongoza ligi kwa pointi 1 na tuna mechi 2 mkononi. Nilishasema Simba itachukua Ubingwa kwa miaka 10 mfululizo.
“Tangu mwaka 1970 hakuna klabu yoyote iliyochukua Ubingwa mara 4 mfululizo, Simba anakwenda kuvunja rekodi mwaka huu baada ya miaka 40, umri wa kugombea Urais. Na tunavunja rekodi ya kufika nusu fainali Klabu ya Mabingwa Afrika,” amesemsa Haji Manara, Msemaji wa Simba Sc.