KIUNGO wa Yanga Mukoko Tonombe amebakiza siku chache kwenda nchini kwao DR Congo katika majukumu ya timu ya taifa lakini ghafla kuna klabu inajipanga kuwasilisha ofa nzito ambayo kama matajiri wa Yanga GSM hawatajipanga anaweza kung’oka.
Klabu ya Horoya AC ndio inayotaka kumchukua Mukoko na Rais wao amethibitisha kwamba Mkongomani huyo ndio silaha yao ya kwanza wanayotaka kuboresha kikosi chao.
Utakumbuka Horoya ambao ni mabingwa wa Guinea ndio walioipokonya silaha ya mabao Yanga wakimnunua mshambuliaji Heritier Makambo kwa dau la Euro 70,000.
Makambo wakati huo alikuwa silaha kubwa Yanga akiwa mfungaji bora wa timu hiyo.
Taarifa kutoka Guinea ni kwamba klabu hiyo inataka kumnunua Mukoko wakimwekea ofa kubwa ya mshahara mara tatu wa ule anaolipwa na Yanga.
Horoya inafahamu kwamba mshahara wa Makambo hauzidi dola 3,100 (Sh6 milioni) pale Yanga na wamemwambia watamlipa dola 9,000 (Sh18 milioni)kwa mwezi.
Achana na mshahara lakini Yanga nao watapewa ofa ya awali ya kiasi cha dola 200,000 kumuachia kiungo huyo aliyebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na Yanga.
Horoya imethibitisha kwamba ofa kamili kwa mabosi wa Yanga itatua rasmi mapema wiki hii lakini pia itategemea kama Yanga itakubali kumuachia ingawa inaelezwa kiungo huyo anaweza kutumia kipengele kimoja cha kuweza kuifanya Yanga kusikiliza ofa hiyo.
Msikie bosi wa Horoya
Rais wa Horoya, Soufiane Souare amethibitisha kumuhitaji Makambo wakisema kwanza wanataka kusikikuwasikiliza Yanga juu ya utayari wa kumuachia kiungo huyo lakini akimsifia ni mmoja kati ya viungo bora wanaowahitaji.
“Tunamjua Mukoko ni kiungo bora pale Yanga lakini pia pale Congo ni mmoja kati ya viungo bora ambao timu yoyote ingependa kuwa naye lakini hatuwezi kumzungumzia zaidi mpaka kwanza tuwatafute Yanga juu ya hilo,” alisema Souare ambaye ni mtoto wa bosi mkuu wa Shirikisho la Soka la Guinea, Antony Souare.
Meneja wa Mukoko
Meneja wa Mukoko, Nestor Mutuale amethibitisha kuwa ni kweli Horoya wanamtaka Mukoko lakini kwanza ni lazima wazungumze na Yanga ili waridhie kila kitu.
“Horoya ni moja tu ya klabu inayomtaka Mukoko lakini sasa ni mapema kuliongelea mimi zaidi ya Yanga wenyewe,” alisema Mutuale.
“Tumewaambia wawatafute kwanza Yanga hasa Rais wa GSM Ghalib Mohamed na Mwenyekiti wa Yanga Dk Msolla (Mshindo) wao ndio wenye uamuzi wa mwisho mimi kazi yangu ni kusimamia haki za mchezaji tu.”
Hata hivyo, ugumu wa Horoya utatokana na Yanga endapo wataamua kuweka ngumu kama ambavyo Horoya iliwahi kuwawekea ngumu Yanga ilipotaka kumrudisha Makambo.