Home Simba SC TRY AGAIN : MSIMU UJAO SIMBA SC TUTAKUWA NA KIKOSI BORA ZAIDI

TRY AGAIN : MSIMU UJAO SIMBA SC TUTAKUWA NA KIKOSI BORA ZAIDI


SIMBA walishachomoka kwenye hatari ile ya kufungiwa na FIFA kusajili katika sakata la beki wao wa zamani, Asante Kwasi, na wamesisitiza kwamba kishindo kinakuja kwenye kuimarisha maeneo manne muhimu.

Wameweka wazi wanachokifikiria kwenye usajili mpya, Ligi Kuu Bara, Kombe la FA pamoja na mashindano ya kimataifa msimu ujao yanayotazamiwa kuanza tena Novemba mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema jana kuwa tishio la adhabu ile ya kufungiwa kusajili lilishaondoka baada ya kumlipa chake beki huyo wa kushoto raia wa Ghana na mikakati mipya imeshaanza kwa ajili ya msimu mpya kimataifa baada ya kufanikisha malengo ya msimu huu ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ilifanya vyema nyumbani iliposhinda 3-0 dhidi ya Kaizer Chiefs katika robo fainali lakini haikufanikiwa kupita kutokana na kutofanya vizuri ugenini katika mechi ya awali walikolala 4-0 Afrika Kusini.

Try Again alisema: “Bado tuna kiu ya kufanya vizuri na kufika mbali zaidi ya hatua hii ambayo tumeishia sasa, tunakwenda kujipanga na kuboresha kikosi chetu kwa ajili ya mashindano haya,” alisema Try Again na kusisitiza kwamba kulingana na mapendekezo ya kocha Didier Gomes watafanya mabadiliko uwanjani katika maeneo machache na kuja na kikosi bora zaidi kitakachopambana zaidi msimu ujao.

Alisema baada ya kushindwa kufikia nusu fainali, wamepania kubeba ndoo ya Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho (ASFC) na hilo linawezekana kwa aina ya kikosi walichonacho na malengo waliyojiwekea msimu huu.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez alisema malengo ya Simba katika mashindano hayo ya kimataifa ni makubwa mno na bado wapo katika vita ya kufanya vizuri zaidi.

“Makosa ambayo tuliyafanya katika mechi ya ugenini katika mechi na Kaizer, wala hayatajitokeza tena na wataweka plani sahihi kwa msimu ujao ili kuwa imara,” alisema Barbara na kuwataka mashabiki wa Simba kuwa karibu na timu yao wakati wao kama viongozi wakiendelea na mipango thabiti.

SOMA NA HII  AHMED ALLY : - KUBEBEA UBINGWA NI FARAJA KWETU..LAKINI KUMFUNGA YANGA KESHO NI FURAHA KUBWA ....

Katika ligi Simba ndio vinara wakiwa na pointi 61, huku wakibakiwa na michezo tisa wakati katika Kombe la ASFC, wapo robo fainali na watacheza leo Jumatano dhidi ya Dodoma Jiji.