Home Ligi Kuu SIMBA SC NA YANGA SC ZAPANGIWA TAREHE MPYA

SIMBA SC NA YANGA SC ZAPANGIWA TAREHE MPYA


YANGA, Simba, Azam na klabu zote za Soka Tanzania Bara zilipangiwa kuanza usajili mpya wa wachezaji kuanzia Juni 15 mwaka huu, yaani wiki mbili zijazo lakini watalazimika kusikilizia tarehe nyingine.

Bodi ya Ligi nchini (TPLB), imetoa sababu mbili za kusogeza usajili huo msimu ujao, ingawa haijataja ni lini hadi itakapopangwa tarehe rasmi.

Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almasi Kasongo aliliambia gazeti la Mwanaspoti jana hakuna namna ya kuzuia kusogeza mbele muda wa usajili kuanza na kumalizika tofauti na ilivyozoeleka hapo kabla.

Alitaja sababu hizo ni kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli na yalitangazwa maombolezo ya mwezi mmoja yaliyosababisha shughuli za soka kusimama.

Sababu ya pili ni ushiriki wa Simba na Namungo FC kwenye michuano ya Caf, hivyo ikaingilia ratiba ya ligi itakayoendelea hadi muda ambao ndio usajili ulitakiwa ufanyike na ligi kuu itamalizika Julai 18.

Kasongo alisema; “Hakuna jinsi usajili kwa ajili ya msimu ujao tutausogeza mbele kidogo ili uendane na muda wa kumalizika kwa ligi yetu, hiyo yote ni kutokana na mambo yaliyokuwa nje ya uwezo wetu.”

Wakati dirisha hilo likisogezwa mbele, baadhi ya makocha wamesema linaweza kuathiri maandalizi ya timu.

Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza alisema hilo la usajili huku ligi ikiwa inaendelea liliwahi kutokea Kenya na mechi zilikosa msisimko.

“Wanatakiwa kuliangalia hilo ikiwezekana kulibadilisha au kusogeza mbele, jambo hilo pia wanatakiwa kuliangalia hata katika mechi za playoff sioni kama timu za FDL zitakuwa salama,” alisema.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Mohamed Badru alisema; “Haiwezekani kocha akawa na umakini, kufanya usajili, kuandaa timu kwa ajili ya msimu ujao, kuibakiza timu, lakini hata timu za FDL hazitakuwa katika hali ya ushindani kama wale ambao wanatoka kwenye ligi kuu.”

SOMA NA HII  RATIBA YA VIPORO LIGI KUU BARA IPO NAMNA HII