Home Simba SC HII HAPA JUMLA YA MABILIONI WALIYOPATA SIMBA SC KUTOKA CAF MSIMU HUU...

HII HAPA JUMLA YA MABILIONI WALIYOPATA SIMBA SC KUTOKA CAF MSIMU HUU TU


MAJONZI ya kutolewa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika bado hayajaisha kwa mashabiki wa Simba lakini kwa hapo ilipofikia haijaaga kizembe na imeondoka na neema kibao ambazo pia zimeinufaisha hata nchi kwa upande mwingine.

Jumamosi iliyopita, Simba ilijikuta ikitupwa nje kwenye michuano hiyo kwa kipigo cha mabao 4-3 licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 matokeo ambayo hayakutosha kupindua matokeo ya kufungwa mabao 4-0 ugenini huko Afrika Kusini.

Lakini pamoja na kutolewa hatua hiyo, Simba imeacha alama ambayo bila shaka itafanya mashabiki wake watembee kifua mbele kutokana na neema zilizoenda sambamba na hatua waliyofikia.

Neema ya kwanza ambayo imetokana na Simba kutinga hatua hiyo ni kuvuna kitita cha Dola 650,000 (Sh 1.5 bilioni) ikiwa ni mara ya pili wanafanya hivyo kama walivyofanya msimu wa 2018/19.

Neema ya fedha hizo haijatua kwa Simba tu bali imeenda hadi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo lenyewe limevuna 5% ya fedha hiyo ambayo Simba imepata.

5% ya Dola 650,000 (Sh 1.5 bilioni) ambayo TFF watapa ni takribani Dola 14,011 (Sh 32.5 milioni).

Ukiondoa suala la fedha, Simba pia imetoa mchango mkubwa katika kuwezesha Tanzania kuwakilishwa na timu nne kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu ujao kutokana na idadi kubwa ya pointi ambazo imevuna kwa kufika hatua hiyo.

Tanzania imepata fursa ya kuingiza timu nne msimu ujao kwa vile ipo kundi la nchi 12 zenye idadi kubwa ya pointi ambazo kiutaratibu zinapewa nafasi ya kuwakilishwa na timu nne msimu unaofuata.

Katika orodha ya nchi na jumla ya pointi ambazo kila moja imekusanya, Tanzania iko nafasi ya 12 ikiwa imekusanya jumla ya pointi 27.5

Simba imetoa mchango mkubwa kuifanya Tanzania ifikishe pointi hizo kwani yenyewe imechangia jumla ya pointi 24, Namungo ikichangia pointi 2.5 na Yanga imechangia pointi moja.

Pia Simba imetoa wachezaji bora wa wiki wa mashindano hayo mara tatu ambapo wa kwanza alikuwa ni Luis Miquissone, akifuatiwa na Clatous Chama na baada ya hapo akashinda John Bocco.

SOMA NA HII  LUIS MIQUISSONE AWEKEWA OFA MBILI, AL AHLY YAWEKA DAU LA MAANA

Kocha wa Simba, Didier Gomes Da Rosa alisema kuwa ana imani kubwa mashindano ya msimu huu yamewapa darasa ambalo litawasaidia kuwa bora zaidi msimu ujao.

“Malengo yetu yalikuwa ni kufika hatua za juu za mashindano haya lakini kwa bahati mbaya tumeshindwa kuyatimiza, naamini tunaelekea pazuri na siku za usoni tutafanya vizuri zaidi.

Jambo kubwa na la msingi ni kujipanga zaidi na kufanyia kazi maeneo tuliyoonyesha upungufu ili tuweze kufika katika hatua za juu zaidi na ikiwezekana kutwaa ubingwa,” alisema kocha huyo raia wa Ufaransa.

Nahodha wa Simba, Bocco alisema mashindano hayo yamewapa kiu na hamasa ya kufanya vyema siku za usoni.

“Hatujafurahia kutolewa kwani tulikuwa na malengo ya kufika mbali lakini hayo yamepita sasa tunarudi kujipanga, tunaamini msimu ujao tutakuwa na nafasi ya kurekebisha makosa yetu na kufika mbali zaidi,” alisema straika huyo mkongwe.