Home Simba SC WACHEZAJI SIMBA WAAPA ‘KUIRARUA’ YANGA ,JUMAMOSI

WACHEZAJI SIMBA WAAPA ‘KUIRARUA’ YANGA ,JUMAMOSI


PRESHA ya pambano la watani wa jadi kati ya Simba na Yanga, ambalo litapigwa Jumamosi Mei 8, 2021 limezidi kupanda huku kila shabiki wa timu hizo akiamini ushindi upo upande wake.

Nyota wanne wa kikosi cha kwanza Simba, wakiwemo Clatous Chama na Luis Jose Miquissone wamekula kiapo kwamba ni ushindi kwanza mengine baadaye.

Kiungo Mzambia Clatous Chama alisema; “Tunahitaji ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kujihakikishia ubingwa wa ligi msimu huu kama malengo yetu ambayo tulijipangia mwanzo wa msimu.”

Katika ligi, Chama amehusika kwenye mabao 20 katika mechi 25 za Simba akifunga saba na kutoa pasi za mwisho 13, huku akivunja rekodi ya msimu uliopita ambao alifunga mabao mawili na kutoa asisti 10.

Mshambuiaji Chriss Mugalu, alisema; “Tunakwenda kufanya maandalizi ya kutosha na wale wachezaji ambao watapata nafasi ya kuiwakilisha timu katika mechi hiyo watapambana vya kutosha ili tuweze kupata ushindi kwani hilo linawezekana.” Mugalu kwenye ligi amefunga mabao manne.

Winga wa Simba, Luis Miquissone alisema msimu huu wamecheza mechi nyingi kubwa ambazo wamepata matokeo mazuri hivyo morali hiyo wamepanga kuihamishia katika mchezo huo dhidi ya Yanga.

“Lazima utakuwa mchezo mgumu kwani tunakutana na timu ambayo tunajuana nayo, inahitaji pointi tatu kutoka kwetu ila kwa aina ya maandalizi ambayo tutayafanya na kikosi chetu kilivyo naona tutapata ushindi,” alisema Miquissone ambaye ni raia wa Msumbiji.

Katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, Miquissone ndio anaongoza kufunga mabao katika kikosi hicho akiwa na matatu wakati katika ligi amefunga nane.

Kiungo Rally Bwalya alisema mechi ya dabi kama hiyo dhidi ya Yanga kwenye nchi yoyote ile huwa inabadilika kama ilivyokuwa katika mechi ya kwanza iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, walikuwa na matumaini makubwa ya kuondoka na ushindi lakini mchezo ulibadilika.

Kwa upande wa kiungo wa Simba, Erasto Nyoni alisema haitakuwa mechi rahisi, hivyo wanajipanga kulingana na mchezo husika kuhakikisha wanapata pointi zitakazokuwa zinaendelea kuwaimarisha kileleni.

SOMA NA HII  MOSES PHIRI AFUNGUKA SABABU YA KUICHINJA YANGA NA KUTUA SIMBA...ADAI HANA MPANGO KUWA MCHEZAJI BORA...

Alisema kila mchezaji Simba anatambua umuhimu wa mchezo huo na kila mchezo ambao watakutana nao kuelekea lala salama hii ya Ligi Kuu akiamini watapambana kupata matokeo ili wazidi kuwapa burudani mashabiki wao.

“Mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga, Simba hatuna kazi ndogo, tunahitaji kuweka heshima ya kuchukua ubingwa kwa mara nne mfululizo, ndio maana kila mechi kwetu tunaichukulia kama fainali,” alisema.