UONGOZI wa klabu ya Simba umefunguka kuwa, hauna pingamizi lolote la kumrudisha aliyekuwa Mkata umeme wao raia wa Brazil, Gerson Fraga Vieira ikiwa tu kocha mkuu wa timu hiyo, Didier Gomes atapendekeza usajili wake.
Mkata umeme huyo aliyehudumu ndani ya kikosi cha klabu ya Simba kwa msimu mmoja wa 2019/20 alipata majeraha ya goti mwanzoni mwa msimu huu na kulazimika kufanyiwa upasuaji wa goti Novemba 25, mwaka jana, ambapo Jumatano iliyopita alitakiwa kufanya vipimo vya mwisho vya MRI, kwa ajili ya kutoa ripoti ikiwa tayari amepona kabisa au la.
Licha ya kumalizana na Simba, Fraga ameendelea kuonyesha mapenzi na sapoti kwa klabu hiyo hususani kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram.
Baada ya Simba kutolewa na Kaizer kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Fraga aliwatumia ujumbe wachezaji wa Simba uliosomeka: “Tugange yajayo, najua marafiki zangu wamejitoa kwa asilimia 100 najisikia fahari kuwakilishwa na kila mmoja wa kaka zangu.”
Akizungumza kuhusu uwezekano wa kumrudisha mkata umeme huyo mkuu wa maudhui wa klabu ya Simba, Ally Shatry amesema: “Kuhusiana na Fraga tayari tulifikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha mkataba kutokana na sababu mbalimbali.
“Lakini hii haimaanishi kwamba hatuwezi kumsajili, kwa kuwa yupo katika hatua za mwisho za kupona anaweza kusajiliwa na kurejea Simba, kama tu atakuwa pendekezo la bendi la ufundi kupitia ripoti ya kocha mkuu, Didier Gomes kwa kushirikiana na kamati ya ufundi ya klabu yetu.
“Ni wazi Fraga mwenyewe bado anaonekana kuwa na mapenzi makubwa na klabu hii na ndiyo maana mara kwa mara amekuwa akitutumia ujumbe wa kututakia kheri na hata kuchapisha picha kwenye mitandao yake ya kijamii akiwa na jezi ya Simba.”