IMEELEZWA kuwa, kiungo mchezeshaji wa Azam FC, Abubakary Salum ‘Sure Boy’ amegoma kuongeza mkataba wa kuendelea kukipiga hapo huku Yanga ikitajwa.
Yanga si mara ya kwanza kuonesha nia ya kuhitaji saini ya kiungo huyo, lakini wamekuwa wakigonga mwamba kwenye ishu ya mkataba alionao ndani ya Azam.
Kuelekea msimu ujao, Yanga imepanga kukiboresha kikosi chake na kati ya sehemu ambayo wamepanga kusajili ni kiungo namba nane ambayo Sure Boy anaicheza.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari, kiungo huyo mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo amegoma kuongeza mkataba mwingine wa kuendelea kubaki Azam.
Chanzo hicho kilisema kuwa, Sure Boy amegoma kuongeza mkataba baada ya kufanya mazungumzo na Yanga.
Kiliongeza kuwa, kama mazungumzo yakienda vizuri kati ya kiungo huyo na mabosi wa Yanga, basi atasaini mkataba kuelekea msimu ujao.
“Katika msimu uliopita viongozi wa Yanga walishindwa kuipata saini ya Sure Boy kutokana na kubanwa na mkataba ambao unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
“Azam walitumia nguvu kubwa kulazimisha abaki kwao katika msimu uliopita, licha ya mwenyewe kuomba aondoke katika timu hiyo ili atue Yanga.
“Katika kuelekea usajili wa msimu ujao, Yanga imeonekana kupania kukiboresha kikosi chao, hivyo upo uwezekano mkubwa wa kumpata Sure Boy baada ya kumkosa msimu uliopita,” kilisema chanzo hicho.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli, juzi alisema: “Sababu kubwa ya kumleta kocha Nabi (Nasreddine) mapema ni kwa ajili ya kuangalia wachezaji katika ligi na kama ikitokea amependezwa naye, basi atatoa mapendekezo ya usajili kwa uongozi.
“Wapo wachezaji ambao tayari wamependekezwa na kocha, hivyo viongozi unaendelea kuwafuatilia kwa karibu kujua uwezo wao kabla ya kuwasajili.”