HUU ndio wakati wa usajili, wakati ambao wachezaji wanaangalia neema kwa ajili ya maisha yao. Klabu zinakuwa zinaangalia zitampata nani kwa ajili ya kuwasaidia kwa ajili ya msimu ujao.
Klabu zinataka msaada kwa maana ya yule ambaye zinaamini ni bora lakini mchezaji anahitaji maslahi kwa kuwa kazi ya uchezaji ni ya muda mfupi sana.
Hivyo kunapokuwa na maslahi lazima ayachangamkie, hili liko wazi. Tayari tuna taarifa ya beki wa kushoto wa Ruvu Shooting, Charles Manyama kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba kwa ajili ya msimu ujao.
Lakini kuna taarifa nyingine kwamba Manyama anakuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kuanza kuleta changamoto kwenye suala la usajili baada ya kuwa kwenye mvutano ambapo habari za awali zilieleza kwamba amemalizana na Simba kisha Azam FC wao wakamilza kazi kwa kumambulisha kabisa.
Usajili huwa inakuwa ni siri kubwa kwa timu zote jambo ambalo limefanya Azam FC wakamilishe mchakato huo ikiwa ni mwanzo kabisa kabla dirisha la usajili halijafunguliwa.
Siri inafanya kuwe na ugumu wa ukweli kupatikana mapema na wakati mwingine wapasha habari wenyewe wanakuwa wagumu sana. Lakini inaonekana kuna shida kidogo katika huu usajili, acha muda utatueleza.
Sijawa na uhakika kwa Manyama kwamba amemalizana na Simba au itakuwa Azam FC lakini ukweli upo hivi, kwake amekuwa kijana anayepanda kwa kasi kubwa sana kimafanikio na ndani ya misimu mitatu tu amekuwa gumzo sana na unaona akitokea Namungo FC hadi Ruvu Shooting na sasa huyo, itakuwa Simba au Azam FC.
Wakati akipambana katika lile suala la maslahi, Manyama anapaswa pia kuwa makini na kujifunza kwamba anapoangalia wapi atapata maslahi makubwa lakini pia aangalie nafasi yake ya kucheza au imani yake ya kuamini.
Moja ni maslahi sahihi kabisa lakini anapokwenda, nafasi ipo vipi,anayekwenda kuchuana naye ni nani na uwezo wake upo vipi na tatu ni ile imani kuwa anaweza vipi kupambana.
Kupambana ni jambo kubwa zaidi, kama unaona uko tayari unaweza kwenda kokote ingawa wakati mwingine pamekuwa wakipoteza wengi na mfano mzuri unamuona Gadiel Michael ambaye kwa muda mfupi tu wa misimu mitatu ameweza kuweka rekodi ya kucheza klabu zote kubwa tatu za Tanzania na sasa yuko Simba akiwa hana uhakika wa namba ya kuanza hata kidogo.
Alitokea Azam FC kwenda kujiunga na Yanga na akawa mmoja wa wachezaji bora, baadaye akaondoka Yanga na kujiunga Simba, mambo hayakuwa mazuri na dalili zote kama Simba wakimpata mbadala wake basi safari itakuwa imewadia kwake.
Maana yake kama Gadiel aliangalia suala la maslahi pekee, sasa unakuwa ni ule wakati mgumu kwake wa kuanza kushuka. Wakati angeweza kubaki timu fulani akapandisha zaidi thamani na ubora wake na angekwenda Simba akiwa tayari haswa.
Unajiuliza, kwa sasa akiondoka Simba, Yanga watampokea? Azam FC watamuona anafaa tena au ndio atakwenda kujiunga na Ruvu Shooting kuziba pengo la Manyama?
Kwa mchezaji hii tayari inaweza kuwa ile hali ya kumchanganya na kumyima nafasi ya kurejea katika kile kiwango chake bora cha utendaji na mwisho ni kuporomoka kabisa na kuanza kuonekana ni mchezaji wa kawaida kabisa.
Kwa umri wa Gadiel kuonekana ni mchezaji wa kawaida lazima hali hiyo itammaliza kabisa kiuchezaji na kumuondoa relini. Na hiki ndicho ninataka kumkubusha Manyama kwamba ana haki ya kuangalia suala la maslahi kwa kuwa anatafuta maisha lakini bila ya ubishi anapaswa kuwa na hesabu ndefu
na za uhakika kwa ajili ya kuangalia maisha yake ya baadaye katika mchezo wa soka.
Yote haya yanawezekana kwa kufanya mambo kwa utulivu bila ya pupa lakini pia kuepuka miluzi mingi sana kwa kuwa wakati mwingine humpoteza mbwa!
Kwa kuwa ametambulishwa ndani ya Azam FC kwa kupewa dili la miaka mitatu basi ana kazi ya kuendelea pale ambapo ameishia ili kuwa bora zaidi.