NYOTA wa Azam FC Prince Dube ambaye amekosekana kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Bara huenda leo Juni 26 akaibukia Uwanja wa Majimaji, Songea kumenyana na Simba.
Azam FC itamenyana na Simba kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho na mshindi wa leo atamenyana na Yanga iliyokata tiketi ya kutinga hatua ya fainali baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Biashara United.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa Dube anaendelea vizuri na anaweza kuanza ikiwa ripoti ya daktari itaeleza kuwa yupo tayari.
“Kuhusu Dube ni kwamba yupo tayari kwa ajili ya mchezo kwani hakuwa ni majeruhi bali alikuwa anaumwa. Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wetu wa robo fainali alitumia dk 10 dhidi ya Rhino Rangers aliumwa tumbo.
“Baada ya hapo aliweza kukosekana kwenye mchezo dhidi ya Gwambina FC na Namungo haina maana kwamba alikuwa hayupo sawa hapana bali dawa alizokuwa anazitumia zilikuwa bado hazijaisha mwilini.
“Ikiwa daktari atasema kwamba anaweza kucheza basi inawezekana hivyo mashabiki wasiwe na mashaka kila kitu kipo sawa,” amesema.