Home CAF AL AHLY: HATUJAMWAJIRI MOSIMANE KWA AJILI YA NGOZI YAKE NYEUSI

AL AHLY: HATUJAMWAJIRI MOSIMANE KWA AJILI YA NGOZI YAKE NYEUSI


RAIS wa Al Ahly, Mahmoud El Khatib amemsifu Pitso Mosimane, akimfananisha na almasi ambayo inastahili mkataba mpya.

Kocha huyo ametisha tangu ametua kuifundisha Ahly inayofahamika pia kama Mashetani Wekundu, akishinda makombe manne na klabu hiyo hadi sasa, na Rais huyo amesema hakuna aliyemuamini Msauzi huyo.

“Niliiona almasi kule Afrika Kusini, nikaenda kuileta hapa, wakati ambao hakuna aliyemuamini Pitso Mosimane. Bodi ilivutiwa sana na dili hili,” alisema El Khatib baada ya timu hiyo kutwaa taji la CAF Super Cup kwa kuifunga RS Berkane 2-0 Ijumaa iliyopita.

“Mara ya kwanza nilipoiona almasi yangu hii, timu yangu ilikuwa imekaa miaka sita bila ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika. Nilipomleta hapa Cairo, milango ya Afrika ikafunguka na ameleta mikononi mwangu medali tulizozitaka za Afrika.

“Najua nyumbani Misri wale wenye roho za kwanini wamechukia kwa sababu Mosimane kwa mara nyingine ameendelea kuleta mataji, sio moja, sio mawili, sio matatu bali manne mikononi mwangu. Kufikia sasa hakuna ninachomdai, ni yeye anayenidai mkataba mnono,” El Khatib aliendelea.

“Hapo kabla hapakuwahi kuwa na klabu iliyowahi kuifunga Ahly mabao 5-0 katika Ligi ya Mabingwa (lakini Mamelodi Sundowns walifanya hivyo 2019 kwenye robo fainali ambacho kilikuwa kipigo kikubwa zaidi katika historia ya Ahly) na Mosimane tu aliyefanya hivyo.

“Nilipomuajiri, niliajiri akili yake, sio mambo ya rangi ya ngozi yake. Najua Qatar wameiona almasi yangu hii na naamini hakuna wezi wa kuja kuniibia.”

SOMA NA HII  KOCHA WA ORLANDO AFUNGUKA WALIVYOTAKA KUMSAJILI SADIO KANOUTE...AMTAJA ONYANGO...