Home Uncategorized STARS YAPEWA RAI YA KUCHUKUA KIKOMBE MISRI, LAZIMA IFUATWE

STARS YAPEWA RAI YA KUCHUKUA KIKOMBE MISRI, LAZIMA IFUATWE


AKILI na mawazo ya mashabiki wengi wa soka hapa nchini vyote vimehamia nchini Misri ambako michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) inatarajiwa kuanza leo Juni 21, mwaka huu.

Kila mmoja hapa nyumbani naamini atakuwa akifuatilia kwa kina namna timu yetu ya taifa, Taifa Stars itakavyokuwa inafanya kwenye michuano hiyo tunayoshiriki kwa mara ya pili baada ya awali kushiriki mwaka 1980.

Imani kubwa ya mashabiki wa Tanzania ipo kwa timu yao hiyo kufanya vizuri ambapo tayari Taifa Stars iliyopo Kundi C na timu za Senegal, Kenya na Algeria, ipo Misri na imekuwa ya kwanza kufika nchini humo.

Kwa mechi mbili ngumu na nzuri za kirafiki ambazo Taifa Stars wamecheza, zinaleta taswira ya kikosi cha ushindani ambacho tupo nacho kwa sasa kuelekea kwenye michuano hii ya Afcon.

Rai yangu kwa wachezaji wote wa kikosi cha Taifa Stars kutambua kwamba kwa sasa hakuna chaguo lingine ambalo mashabiki wengi wanalitaka zaidi ya kutarajia maajabu kwenu kwenye michuano ya hiyo.

Kikubwa ambacho kinatarajiwa kwa sasa ni kuwatoa kimasomaso mashabiki ambao wengi wapo nyuma yenu wakiwasapoti. Hakikisheni mnawapa matokeo chanya wale wote wanaowasapoti.

Ikumbukwe kuwa matokeo chanya hayaji kimiujiza, bali yanatafutwa ndani ya uwanja bila kutazama aina ya timu ambayo mnacheza nayo, mnatakiwa kujiamini kwamba mnaweza kufanya kweli kwa kila timu mtakayopambana nayo.

Kwa kila mchezaji atakayepata nafasi ya kuingia ndani ya uwanja, anatakiwa aonyeshe uwezo wake wote katika kulipigania taifa lake la Tanzania.

Asifanye majukumu kwa namna anavyojisikia, lazima afanye kwa kujitoa kwa manufaa ya taifa lake akiwa na uchungu ndani ya moyo wake mwenyewe kwamba akipoteza mechi aone kama amepoteza kitu chake cha thamani kubwa.

Jeshi lenu moja la maangamizi, hivyo silaha zenu zote mzitumie kwa manufaa ya timu bila kuhofia namna gani ambavyo mnakwenda kupambana uwanjani, hivyo uhakika wa kupata matokeo chanya upo mikononi mwenu.

Mkiwa ndani ya uwanja kumbukeni kwamba Watanzania wanawategemea ndio maana wapo nanyi bega kwa bega, hilo msiliwaze, kuhusu sapoti wengi tupo nyuma yenu tukiwaombea dua mfanye vema kwenye michuano hiyo ya Afcon.

Mashabiki wa Tanzania wanapenda mpira, hivyo mlitambue hilo wachezaji mkiwa ndani ya uwanja, msiwaangushe mashabiki wakati wenu wa kuonyesha imani ni sasa.

Mdogomdogo mashabiki watarejea kwenye ubora wake endapo mtaanza kufanya kweli hasa ukizingatia kwamba wapo baadhi ambao kidogo wameanza kukata tamaa jambo ambalo sio sawa kulifanya kwa timu yetu.

Kwa wale ambao wamekata tamaa napenda kuwapa moyo kwamba timu yetu ya taifa ina uwezo mkubwa hasa ukitegemea namna walivyo na muunganiko mzuri wa wachezaji kwa sasa.

Nilipata nafasi ya kutazama mchezo wa kwanza dhidi ya Misri ambao ulikuwa wa kirafiki niligundua mengi sana ya kiufundi ambayo yameboreshwa na yanaleta raha kuyatazama kwani licha ya kufungwa bado kuna kitu kilikuwa kinaonekana.

Sehemu ya ulinzi hasa ndiyo inatakiwa ifanyiwe mikakati mikubwa pamoja na eneo la kiungo kwani wamekuwa na tatizo la kushindwa kupeleka mipira katikati, huku ulinzi ukipoteza nguvu kwa upande wa mlinda mlango.

Ni wakati sahihi kwa Aishi Manula kujitoa, awe anazungumza na walinzi wake pamoja na timu nzima, ili kuhakikisha na yeye kazi yake inakwenda vizuri.

Benchi la ufundi ni muda sahihi wa kufanya maboresho hasa kupitia makosa ambayo yametokea kwenye mechi mbili ikiwa ni pamoja na ile dhidi ya Zimbabwe iliyomalizika kwa sare ya 1-1.

Ushindani ni mkubwa, hilo haliwezi kupingika ndio maana yakaitwa mashindano, hivyo Watanzania tuna imani na Taifa Stars nanyi, hakikisheni mnatulipia imani yetu hiyo kwa kufanya maajabu ya kweli tena yale ya ushindi siyo kuboronga.

Kila la kheri Taifa Stars kwenye maandalizi ya mwisho kuelekea kwenye michuano hiyo, tunawaamini, hivyo msituagushe, fanyeni kweli tu maana hamna namna.

SOMA NA HII  SAMATTA KUIKOSA TUNISIA NOVEMBA 13